Belinda Joseph, Songea – Ruvuma. Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), linatarajia kufanya mkutano mkuu maalumu kuelekea uchaguzi wa viongozi wa jukwaa hilo mnamo Aprili 5, 2025, mjini Songea. Mkutano huu unatarajiwa kuwa muhimu kwa ajili ya uchaguzi wa viongozi wa jukwaa na pia ni sehemu ya mchakato wa kukuza na kuimarisha taaluma ya uandishi wa habari nchini Tanzania. Akizungumza na Waandishi wa Habari leo, Aprili 3, 2025 Mwenyekiti TEF, Deodatus Balile alisema kuelekea uchaguzi huo, wanatarajia kuwa na mkutano maalumu kesho, Aprili 4, 2025. Mgeni rasmi katika mkutano huo anatarajiwa kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na mgombea mwenza urais 2025 kupitia chama hicho, Balozi Dkt Emmanuel Nchimbi. Amesema, “suala la kumualika Katibu Mkuu wa CCM ni sehemu ya utaratibu wao wa kuwaalika viongozi mbalimbali wa vyama na serikali katika mikutano yao. Hii ni kwa lengo la kuonyesha usawa na kujenga umoja, bila kujali itikadi za kisiasa za viongozi hao.”
Alitaja baadhi ya mikutano iliyoshirikisha viongozi kama vile Tundu Lissu na Freeman Mbowe, akisema kuwa Jukwaa la Wahariri Tanzania linajivunia kuwa na ushirikiano na viongozi kutoka pande zote za kisiasa. Balile pia aliwaasa waandishi wa habari kutokuegemea upande wowote wa kisiasa, badala yake kufuata miiko ya kazi yao. Alihimiza waandishi kujiepusha na kujihusisha na kampeni za kisiasa au kuonyesha upendeleo kwa upande wowote wa vyama vya siasa. Alisisitiza kuwa waandishi wanapaswa kuwa wasomi na waadilifu katika kutekeleza majukumu yao.
Katika maelezo yake, pia alikumbusha kwamba Jukwaa la Wahariri Tanzania limekuwa na jukumu kubwa la kukuza taaluma ya uandishi wa habari, akisema kwa mwaka 2022, walifanikiwa kuandaa Mkutano mkubwa wa Afrika wa Vyombo vya Habari (Africa Media Convention) ulioshirikisha nchi 54 za Afrika, uliofanyika jijini Arusha. Pia, aliitaja mikutano ya pili na ya tatu iliyofanyika nchini Zambia mwaka 2023 na Accra, Ghana mwaka 2024. Mkutano mwingine mkubwa wa mwaka huu unatarajiwa kufanyika nchini Morocco.
Aidha, alieleza kuwa Jukwaa la Wahariri Tanzania limekuwa mstari wa mbele katika kuhimiza heshima kwa wanahabari, kuongeza mapato kwa vyombo vya habari na kukuza taaluma. Lengo lao ni kuhakikisha kuwa wanahabari wanakuwa na ustawi na maendeleo katika utendaji wao. Balile pia alieleza kuwa uchaguzi huo unatarajiwa kufanyika Aprili 5, 2025 utahusisha nafasi ya Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na Wajumbe wa Kamati ya Utendaji. Aliwashauri wanachama kuwa na kampeni za kistaarabu na kwa amani, ili kutoa mfano mzuri kwa jamii na kuonyesha njia bora ya kufanya kampeni bila vurugu yoyote.

LAAC yamtaka CAG kufanya ukaguzi maalum Farkwa
Maisha: Kosa langu ni kujiachia na kubeba mimba ya pili