Belinda Joseph, Songea – Ruvuma.
Serikali ya Tanzania imetangaza kutoa muda wa miezi saba kwa Shirika la Viwango la Tanzania (TBS) ili kufanya ukaguzi na ufuatiliaji kwa wazalishaji na wasambazaji wa vyakula muhimu kama unga wa ngano, unga wa mahindi, mafuta ya kula, na chumvi.
Lengo kuu ni kuhakikisha kuwa vyakula vyote vinavyotumika nchini vinakuwa na virutubisho vya lishe, hatua inayotarajiwa kupambana na utapiamlo na kuboresha afya ya jamii. TBS itahakikisha kuwa bidhaa hizi zinakidhi viwango vya afya kabla ya mwezi Disemba mwaka huu.
Uzinduzi wa sheria na kanuni mpya za urutubishaji na makabidhiano ya mashine za urutubishaji ulifanyika tarehe 3 Aprili 2025, mjini Songea, Mkoa wa Ruvuma, ambapo Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud S. Kigahe alizindua rasmi mashine hizo. Mashine za “dosifiers” zitasaidia kuhamasisha jamii kuhusu manufaa ya virutubisho vya ziada katika vyakula.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Kigahe aliwahimiza wazalishaji waendelee kutengeneza vyakula vyenye virutubisho ili kupambana na tatizo la utapiamlo, akieleza kuwa tafiti zinaonyesha kuwa asilimia 37 ya wanawake wa umri wa kuzaa wana upungufu wa damu. Aliongeza kuwa elimu kuhusu mlo kamili ni muhimu kwa afya bora ya kila mtu, kwani afya imara ndiyo msingi wa mafanikio ya kijamii na kiuchumi.
Amesema bidhaa zote zinazozalishwa nchini lazima ziwe na taarifa za virutubisho ili wananchi waweze kufanya uchaguzi bora wa vyakula. Kanuni zilizokamilika Novemba 2024 zitawanufaisha wazalishaji wote, wadogo na wakubwa, na serikali imeendelea kuboresha mazingira ya biashara katika sekta hii muhimu.
Akimwakilisha Waziri wa Afya, Saitole Laizer alikumbusha kuwa mpango wa urutubishaji wa vyakula ulianzishwa mwaka 1994, wakati wa Rais Ali Hassan Mwinyi, ili kuongeza madini muhimu katika chumvi.
Hadi sasa, asilimia 90 ya Watanzania wamefaidika na chumvi hiyo iliyoongezwa madini, na sasa serikali inapania kuongeza virutubisho katika unga na mafuta ili kupambana na changamoto za ngozi na macho.
Laizer aliongeza kuwa, urutubishaji wa vyakula utaisaidia Tanzania kupunguza vifo vya mama na mtoto wakati wa kujifungua, na kuwa serikali inajitahidi kuwafikia waathirika hasa katika maeneo ya vijijini ili kutoa elimu na kupambana na utapiamlo.
Dkt. Luis Chongoko, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, alielezea kuwa tafiti za mwaka 2022 zilionesha kwamba Mkoa wa Ruvuma una watoto elfu 90 wenye udumavu, sawa na asilimia 35.6. Alisisitiza kuwa elimu na ushirikiano wa jamii ni muhimu katika kupunguza tatizo hili na kufikia lengo la kupunguza udumavu kwa asilimia 17.8 ifikapo mwaka 2030.
Shehe wa Mkoa wa Ruvuma, Ramadhani Mwakilima, alisisitiza umuhimu wa usimamizi wa mafuta ya kupikia ili kuhakikisha yanakidhi viwango vya afya, na kuomba elimu zaidi kuhusu matumizi ya folic acid kwa wajawazito ili kuepuka matatizo ya kiafya.
Uzinduzi huu wa sheria za urutubishaji unafanyika chini ya kauli mbiu “Matumizi ya vyakula vilivyoongezwa virutubisho kwa kuimarisha afya na kujenga uchumi,” na unalenga kuboresha afya ya wananchi, kupambana na utapiamlo, na kuhamasisha uzalishaji wa vyakula bora na salama nchini.