Swaum Katambo – Katavi.
Changamoto iliyokuwa ikiwakabili wanafunzi waliokuwa wakitokea umbali mrefu kuelekea katika Shule ya Msingi Sitalike sasa imepatiwa mwarobaini mara baada ya kukamilika kwa Shule Shikizi ya Msingi Igongwe iliyoanzishwa kwa nguvu za wananchi.
Wakizungumza wakazi wa Kata ya Sitalike Halmashauri ya Nsimbo mkoani Katavi wamedai kuwa waliamua kuanzisha ujenzi wa Shule hiyo kutokana na adha walizokuwa wakikumbana nazo watoto wao.
Changamoto hizo ni pampja na kutembea umbali wa zaidi ya kilomita tatu hadi sita huku wakikutana na misukosuko ikiwemo ya wanyama wakali kama tembo na viboko wanaotokea katika hifadhi ya Taifa Katavi.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Nsimbo, Daniel Walakunga amesema wameungana na Mbunge wa Jimbo la Nsimbo katika ziara ya ukaguzi wa miradi mipya ikiwemo ya Shule hiyo pamoja na mradi wa nyumba za walimu Shule ya Msingi Jilabela uliopo Kata ya Itenka.
Hata hivyo, mara baada ya kuweka jiwe la msingi na kuzindua miradi hiyo miwili Mbunge wa Jimbo la Nsimbo, Anna Lupembe amesema Serikali ilitambua umuhimu wa uwepo wa Shule hiyo.
Amesema iliongeza fedha kwa ajili ya kuunga mkono juhudi za Wananchi hao huku wakiahidi kutoa fedha nyingine kwa ajili ya kumalizia maradasa yaliyobaki.