Belinda Joseph, Songea – Ruvuma.
Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi na Mgombea Mwenza Urais, Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, amewataka wahariri wa vyombo vya habari pamoja na waandishi wa habari kuzitumia kalamu zao vizuri ili kuchochea amani, utulivu, na kuongeza umoja katika jamii, badala ya kuzusha vurugu.
Ametoa wito huo leo mjini Songea, mkoani Ruvuma, akiwa mgeni rasmi katika Mkutano Mkuu Maalumu wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), kuelekea uchaguzi wa viongozi wa jukwaa hilo, ambapo kesho Aprili 5, 2025, watachagua Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, na wajumbe wa Kamati ya Utendaji wa jukwaa hilo.
Balozi Nchimbi amepongeza kazi kubwa zinazofanywa na wahariri katika kuzitangaza 4R za Rais Samia Suluhu Hassan, ambazo sasa jamii imeanza kuzielewa, na kusema ni dhahiri kwamba wananchi wanatambua umuhimu wa vyombo vya habari. Ameiomba TEF kuendelea kufanya kazi ya kujenga jamii ya Tanzania.
Aidha, amewapongeza wahariri kwa kuwa chujio la habari zote katika taifa, akieleza kuwa endapo wangetumia nafasi zao vibaya, jamii ingekuwa katika hali tofauti na ilivyo sasa.
Balozi Nchimbi alibainisha kuwa Chama cha Mapinduzi kinatambua mchango mkubwa wa vyombo vya habari na dhamira ya chama hicho ni kuhakikisha vyombo hivyo vinafanya kazi kwa uhuru unaoendelevu. Alisema kuwa katika kipindi cha miaka mitatu, Tanzania imepiga hatua kubwa, ikiwa imezipita nchi zaidi ya hamsini kwa kuwa na uhuru wa vyombo vya habari.
Alitaja mihimili mitatu ya serikali – Serikali, Bunge, na Mahakama – na kusema kuwa muhimili wa nne ni vyombo vya habari, ambavyo ni chombo muhimu cha kufanya uangalizi wa mihimili hiyo mitatu kwa kufuatilia mienendo, kukosoa, kushauri, na kutoa mapendekezo ya namna sahihi ya kufikia lengo.
Balozi Nchimbi pia alifurahishwa na ufanisi wa uchaguzi wa viongozi katika jukwaa hilo la wahariri, ambalo linafuata matakwa ya kidemokrasia kila baada ya muda, na kusema kwamba hili linapaswa kuwa mfano kwa taasisi nyingine na kwamba taasisi zisizofanya uchaguzi zinakosa maendeleo na baadhi zinaweza kufa kabisa.
Akizungumza wakati wa kumkaribisha mgeni rasmi kwa niaba ya Waziri wa Habari, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Khamis Mwinjuma, amesema tasnia ya habari ni muhimu kama mhimili wa demokrasia nchini, hivyo waandishi wa habari wanatakiwa kuendelea kuzingatia maadili ya uandishi wa habari kwa nidhamu ya hali ya juu.
Amesema, kama wizara, wanatambua changamoto za tasnia hiyo na wanaendelea kufanya juhudi za kuzishughulikia. Alisema kuwa katika uongozi wa Rais Samia, ameweza kuimarisha uhuru wa vyombo vya habari kwa kuanzisha Bodi ya Ithibati yenye wajumbe sita, watatu kati yao wakitoka katika Jukwaa la Wahariri Tanzania, ambapo lengo kuu ni kuchochea uhuru wa vyombo vya habari.
Mwinjuma amewataka wahariri, hususan katika kipindi cha uchaguzi mkuu wa mwaka huu 2025, kujitahidi kutenda haki katika kuripoti habari zote ili kulinda amani ya nchi. Amehimiza waandishi wa habari kutoa taarifa kwa usawa bila kuchafua wengine na kuleta ugonvi katika jamii.