Belinda joseph, Songea – Ruvuma.
Deodatus Balile ameendelea kuwa kiongozi wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) kama mwenyekiti wa jukwaa hilo, kufuatia uchaguzi uliofanyika Aprili 5, 2025, Songea Mkoani Ruvuma, ambapo katika nafasi ya uenyekiti alikuwa ni mgombea pekee, aliepitishwa na wajumbe wa mkutano mkuu kwa kishindo kikubwa na hatimaye kuendelea kuitumikia nafasi hiyo kwa kipindi cha pili.
Balile, Mwenyekiti wa TEF, amepongeza wajumbe kumchagua tena kwa heshima ya pekee ya kupita bila kupingwa pamoja na Makamu Mwenyekiti Bakari Machumu, kuiongoza TEF kwa kipindi cha miaka minne ijayo kuanzia 2025 mpaka 2029. Katika umoja wao wataifikisha TEF ilipokusudiwa, amemshukuru Mwenyekiti wa uchaguzi huo Frank Sanga pamoja na Kamati nzima ya uchaguzi iliyosimamia vyema uchaguzi huo na kutoa matokeo kwa uhuru na haki.
Ameahidi kuendelea kushirikiana vyema na Kamati iliyochaguliwa pamoja na wajumbe kwa ujumla, amesema watatangaza nafasi za ajira kwa waliopo na wasio ndani ya Jukwaa hilo ili kuleta ushindani kwani baadhi ya nafasi za ndani ya TEF zinahitaji watu wenye uwezo zaidi wa utendaji kazi na sio kupeana kazi kwa kujuana. Hivyo ni bora wafike wakati waamue kuajiri watu watakaoweza kufanya kazi kwa kasi ya upepo ili kuhakikisha wanafikia malengo waliyokusudia.
Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) limefanya uchaguzi wake mkuu mkoani Ruvuma, na kwa mara nyingine, Deodatus Balile amechaguliwa kuendelea kuwa Mwenyekiti wa jukwaa hilo kwa kipindi cha miaka minne ijayo. Uchaguzi huo umefanyika Aprili 5, 2025, Mjini Songea Mkoani Ruvuma kwa uhuru, haki na amani, huku wajumbe wa mkutano huo ambao ni wahariri kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini wakishiriki mchakato huo kikamilifu.
Kwa mara nyingine, Balile amepewa dhamana ya kuongoza TEF ikiwa ni ishara ya imani kubwa ya wanachama wa TEF kwa uongozi wake, katika kulinda na kukuza maslahi ya wanahabari nchini. Uchaguzi huo ambao ulihusisha pia nafasi ya Makamu Mwenyekiti ambaye alikuwa mgombea pekee Bakari Machumu, amefanikiwa kutetea nafasi yake kwa ushindi mnono.
Akizungumza Makamu Mwenyekiti wa Jukwaa hilo Bakari Machumu, amepongeza uchaguzi huo na kuahidi uchaguzi ujao watakaa na kuona namna ya uhesabu kura wa kidijitali ili kurahisisha mchakato huo, ametoa ombi kwa wajumbe wa mkutano mkuu kushirikiana nae kwa kujaza madodoso ya kukusanya maoni mbalimbali na kubaini ni kwa namna gani tasnia ya habari inakabiliwa na changamoto na jinsi ya kuzitatua.
Mwenyekiti wa uchaguzi Frank Sanga, akisoma orodha ya washindi wa Kamati ya utendaji, amepongeza uchaguzi huo jinsi ulivyoendeshwa akifurahishwa zaidi na namna ambayo wamefanikiwa kuwapata wagombea wa mchanganuo unaotakiwa ikiwemo wa upande wa Zanzibar kwa ajili ya kuenzi na kuendeleza Muungano wa Tanzania.
Amewataja wajumbe waliochaguliwa ambao ni Bakari Kimwaga (kura 114), Salim Said (kura 108), Joseph Kulangwa (kura 107), Stella Brown (kura 99), Tausi Mbowe (kura 98), Anna Mwasyoke (kura 83), na Jane Mihanji (kura 73). Walioshindwa ni Angelina Akilimali (kura 35), Esther Zolamula (kura 39), Reginald Mivuko (kura 47), Yasin Sadik (kura 60), na Peter Nyanje (kura 72).
Wakizungumza, Wajumbe wa Kamati ya Utendaji walioshinda uchaguzi huo, akiwemo Tausi Mbowe, na Salim Said, wamewashukuru wajumbe wote waliowapigia kura na ambao hawajawapigia kura huku wakiahidi kushirikiana nao katika kila jambo na kuwatumikia wanataaluma wa habari, ambao wapo tayari kupokea maoni kwa ajili ya utekelezaji na kuyafanyia kazi yote waliyoyaahidi wakati wa kampeni.
Kwa upande wa wagombea nafasi ya wajumbe wa Kamati ya Utendaji ambao hawakushinda uchaguzi huo, akiwemo Angelina Akilimali na Peter Nyanje, wamewashukuru wajumbe wote waliopiga kura kwa mchakato mzima, wakiahidi kuendelea kushirikiana na TEF pale watakapohitaji msaada binafsi pamoja na kuona namna ambavyo wanavyotegemeana.
Walisema kwamba hakuna wajumbe bila Kamati ya Utendaji (KUT) na hakuna kuti bila wajumbe, hivyo ni muhimu sana kudumisha ushirikiano.
Hitimisho la uchaguzi huu linaonyesha kuwa TEF inaendelea kuwa na viongozi imara ambao wanajitolea kwa dhati kuleta mabadiliko chanya katika tasnia ya habari nchini.
Uongozi wa Deodatus Balile na Bakari Machumu umeonesha imani kutoka kwa wanachama wa TEF, na kwamba juhudi zao za kulinda maslahi ya wanahabari zitakwenda mbali zaidi kwa kipindi cha miaka minne ijayo.
Ushirikiano wao na Kamati ya Utendaji ni muhimu katika kuhakikisha malengo ya jukwaa hilo yanafanikiwa na wanahabari wanaendelea kuwa na sauti yenye nguvu katika jamii.
Uchaguzi huu umeonesha umuhimu wa kuboresha mifumo ya uchaguzi katika TEF, na suala la kutumia teknolojia ya kidijitali ili kurahisisha mchakato linatarajiwa kuwa na manufaa makubwa kwa uchaguzi ujao.
Inaarifiwa kuwa, jambo hilo litasaidia kuongeza uwazi na usahihi wa matokeo, huku ikizingatia maslahi ya wanahabari wote bila kujali jinsia au asili zao.
TEF imesema inajivunia kuwa na viongozi walio na maono ya mbele na azma ya kuendeleza tasnia ya habari nchini Tanzania.