Jitihada za kutangaza bidhaa zinazozalishwa nchini kwa lengo la kuhamasisha matumizi ya bidhaa hizo kupitia mikakati mbalimbali ya Ukuzaji Biashara ndani na nje ya nchi zinaendelea.
Akizungumza hii leo Bungeni Jijini Dodoma, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe wakati akijibu swali la Mbunge wa Muleba Kusini, Dkt. Oscar Ishengoma ambapo aliuliza Je, Serikali ina mpango gani wa kuhamasisha watumiaji wa Tanzania kununua bidhaa na huduma zinazozalishwa hapa nchini.
Amesema, “mikakati hiyo ni pamoja na, Kuanzishwa kwa rajamu/chapa maalumu ya bidhaa ya “Made in Tanzania” ambayo itatumika kwa lengo la kutambulisha na kutangaza bidhaa zinazozalishwa nchini katika masoko yetu ya ndani na pia yale ya Kimataifa.”

“Kuratibu Maonesho ya bidhaa za Tanzania (TIMEXPO) na Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) yanayofanyika kila mwaka, ikiambatana na utekelezaji wa Kampeni ya “Nunua bidhaa za Tanzania, Jenga uchumi wa Tanzania” ambapo wazalishaji, wasambazaji, wanunuzi pamoja na watoa huduma za usaidizi kutoka sekta za umma na binafsi hushiriki,” amesema Kigahe.
Ameongeza kuwa, Serikali itaendelea kuhamasisha matumizi ya bidhaa zinazozalishwa nchini kupitia majukwaa mbalimbali ikiwa ni pamoja na niliyoyataja hapo juu.
“Aidha, niwaombe Waheshimiwa Wabunge kuwa mabalozi kwa kununua na kutumia bidhaa zinazozalishwa na wazalishaji wa ndani na kuhamasisha jamii ya Watanzania kutumia bidhaa hizo,” amesema Kigahe.