Boniface Gideon – Tanga.
Wasomi wa Dini ya Kiislamu mkoani Tanga wakiwemo, Mashekh na Wanazuoni ]wamekemea vikali vitendo visivyo vya kimaadili vinavyofanywa na baadhi ya watu Wasomi waliopo kwenye nafasi za uongozi kwenye taasisi mbalimbali, ikiwemo Wizi wa Mali za Umma, udokozi, ubinafsi na Mfumo mbovu wa mavazi yasiyokuwa na staha.
Aidha Wasomi hao wa Dini wameonya Jamii kama haitochukua hatua kali na madhubuti zaidi ya kwenye malezi bora basi hali itakuwa mbaya zaidi mbeleni.
Wakizungumza jana Jijini Tanga kwenye mahafali ya 15 , kidato cha Sita (6) ya Shule Al-Kheir Islamic Girls Seminary iliyo chini ya Taasisi ya Direct Aid Society, Mohamed Abbas Athuman, Kaimu Mkurugenzi wa Al-Kheir Islamic Girls Seminary ambaye pia ni Msomi na Kiongozi wa Kidini alisisitiza kuwa kwa sasa hali ya maadili ni mbaya zaidi hususani katika kundi la wasomia
“Sasa hivi, unamkuta msomi, hata kabla hajapata ajira anaanza kutajirika, kuna mameneja, wakueugenzi na kila anayepata nafasi ya kuongoza Taasisi ya Umma utamkuta ni tajiri,mtu anaanza kutajirika kabla ya hajaanza Kazi kwenye kitengo ambacho atakitumikia,tunatengeneza kizazi kibovu kisicho na maadili katika Jamii yetu,” alisisitiza Athuman.

Athuman aliwataka Wahitimu hao kwenda kuwa mfano na kufuata maadili ya Kidini waliyofundishwa kwa muda wote waliokuwepo chini ya Taasisi hiyo.
“Naongea na nyie Wanafunzi, mnaenda vyuoni,kwa bahati mbaya zaidi, vyuoni hakuna kuchapwa wala kusimamiwa na Mwalimu, hakuna kuchelewa namba, mtakuwa huru kufanya chochote ukipendacho bila kuulizwa,mtakwenda kuharibikiwa, wengi wanaharibikia huko, niwaombe mkawe mfano kwa Jamii, achaneni na Mambo ya Dunia, zingatieni maadili ya Dini yetu ili tuwe na kizazi bora chenye kumjua Allah,” aliongeza Athuman.
Aliwataka Wazazi kujenga misingi imara zaidi ya malezi kwa njia za Kidini ili kujenga kizazi bora chenye hofu ya Mungu,
“Sisi Wazazi, tujitahidi sana kuwasimamia Watoto wetu, haya tunayoyaona kwenye Jamii yetu ni matokeo ya malezi,ni lazima Watoto wetu walelewe kwa Misingi ya Dini, tukiwa na watu wenye hofu ya Mungu, basi hata huduma kwenye kila ofisi zitakuwa bora zaidi, Wazazi tujitahidi kuwalea Watoto wetu katika Maadili ya Dini,” aliongeza Athuman.
Naye Burhan Yakub, ambaye ni mjumbe wa Bodi ya Shule hiyo Msomi, alisema suala la Maadili ni la Jamii nzima na kila mmoja anapaswa kulisimamia kwa nguvu zote na sio kuwaachia Viongozi wa Dini pekee.

“Suala la Maadili ni la kila mmoja wetu,tunapaswa kulisimamia kwa nguvu zote, tusiwaachie viongozi wa Dini pekee yao,hivyo nyie Wahitimu wetu nendeni mkayazingatie yote tuliyowafundisha hapa, tunataka tuwe na Jamii yenye hofu ya Mungu na kwa hivyo tutapata watumishi bora zaidi katika Jamii,” alisisitiza Burhan.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Taasisi ya Direct Aid Society Ahmed Farhaty, alionya mfumo wa Elimu Nchini , ambapo bidhaa nyingi zinazotoka nje ya Nchi lakini malighafi zake zinatoka Tanzania.
“Ukiangalia bidhaa nyingi tunazotumia majumbani zikiwemo hizi spika na maiki tunazotumia hapa zimetengenezwa nje ya Nchi, lakini malighafi zake zinatoka Tanzania, hii ni hatari sana, Vijana mnaohitimu nendeni mkawe Wabunifu ili Taifa letu lipate kunufaika na Rasilimali zake,” aliongeza Farhaty.