Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel amesema Serikali imefanya utafiti wa kina nchi nzima wa kusaidia kutambua ni saratani zipi zinaongoza katika kanda ya ziwa na kubaini kuwa saratani ya kibofu cha mkojo, mji wa uzazi wa kinamama, damu, macho na figo ndio zinazoongoza.
Dkt. Mollel ameyatanabaisha hayo leo Aprili14, 2025 Bungeni hapa Jijini Dodoma wakatia akijibu swali la Mbunge wa viti maalum Mkoa wa Mwanza, Kabula Shitobela aliyehoji ni lini Serikali itatoa majibu ya tafiti zilizofanywa Kanda ya ziwa kubaini visababishi vya Kansa iliyokithiri.
“Wataalamu wamekusanya sampuli za damu 9600 za watu ambao hawana saratani ili kulinganisha na sampuli za damu za wenye saratani, utafiti huu utasaidia kubaini chanzo cha hizo saratani,” amesema.

Amesema kwa sasa bado utafiti unaendelea na visababishi vinavyosemwa bado ni nadharia tu kutokana na shughuli za kijamii katika maeneo husika.
“Hadi sasa mpango wa kudhibiti ongezeko umejikita katika kutoa elimu ya Afya kwa viashiria vinavyodhaniwa pamoja na kuzingatia Mkakati wa kitaifa wenye maeneo saba yaliyoainishwa ili kudhibiti viashiria vya saratani,” amesema.
Aidha, akijibu swali la nyongeza la Mbunge huyo, lililoulizwa na Mbunge wa Viti Maalum kutoka Mkoa wa Kagera, Neema Lugangira juu ya Wizara kama haioni haja ya Serikali kuwa na chombo maalum cha kudhibiti masuala ya chakula kutokana na uwepo wa shughuli nyingi za sekta ya madini na uchepushaji wa kemikali kwenda ziwa Viktoria na kusemekana kwenda kuathiri samaki na dagaa ambazo jamii inayozunguka ziwa hilo inakula kwani kuna ongezeko kubwa la kuchangia uwepo wa kansa.

Dkt. Mollel amesema kwasasa Serikali inacho chombo cha kusimamia masuala ya chakula ambacho ni TBS, ambapo imekuwa ikifanya kazi ya kina ya kuhakikisha uchafuzi huo unaofanyika unasimamiwa kwa kina.
“Nakubaliana nawewe kwamba bado kuna watu ambao sio wazuri na hawafuati zile sheria ambazo wenzetu wa afya, lakini wenzetu wa mazingira na maji wamezitoa katika kuchepusha vitu mbalimbali ambavyo vinaweza kuwa na madhara kwa kwa binadamu, kwahiyo hilo tutaendelea kuliongezea nguvu katika kufuatilia eneo hilo,” amesema.