Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) imesema itasitisha matumizi ya namba za vitambulisho vya Taifa kuanzia Mei Mosi, 2025 kwa wote waliotumiwa ujumbe mfupi wa maneno na hawakufika kuchukua vitambulisho vyao.
Mkurugenzi Mkuu wa NIDA, James Kaji ameyasema hayo hii leo Aprili 14, 2025 na kuongeza kuwa tangu zoezi hilo lilipoanza Januari 2025 hadi Machi 23, 2025, wananchi 1,880,608 walikuwa bado hawajachukua vitambulisho vyao, na 565,876 walifika kuvichukua ambao ni sawa na asilimia 30.
Amesema, “NIDA imesikitishwa na idadi ndogo ya wananchi wanaojitokeza kuchukua vitambulisho vyao licha ya kutumiwa ujumbe wa kuwataarifu mahali pa kuvichukua. Hivyo tumeamua kusitisha matumizi ya namba za vitambulisho kwa wale waliotumiwa SMS lakini hawajajitokeza.”
Kaji ameongeza kuwa, yeyote akaposajiliwa atapokea ujumbe wa namba yake ya NIDA ndani ya siku tano na kwamba ndani ya siku 21 utatumwa ujumbe mpya kwake kumuelekeza mahali pa kuchukua kitambulisho chake na endapo atashindwa kufika ndani ya mwezi mmoja, namba yake itafutwa.
Aidha, ametoa wito kwa Wananchi kuhakikisha pia wanatunza ujumbe huo na kuenda nao katika ofisi za NIDA walizoelekezwa kupitia ujumbe, ili kupata huduma hiyo kwa urahisi.
“NIDA inafikiria uwepo wa faini kwa wale watakaoshindwa kufuata utaratibu huu, hasa ikizingatiwa kuwa serikali inatumia fedha nyingi kutoa huduma hiyo bila malipo,” alifafanua Kaji.