Tanzania imepanda kwenye viwango vya uhuru wa vyombo vya habari duniani, kutoka nafasi ya 143 mwaka 2023 hadi nafasi ya 97 mwaka 2024 ikichangiwa na 4R za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Habari,Utamaduni, Sanaa na Michezo, Prof. Paramagamba Kabudi jijini Dodoma wakati akizungumza na Waandishiwa Habari juu ya mafanikio ya Wizara hiyo katika kipindi cha miaka Minne ya uongozi wa Rais Samia.

Amesema, “hii inaonesha jitihada za dhati za Rais Samia za kuimarisha sekta ya habari nchini, mpaka kufikia mwezi Machi mwaka huu, Tanzania ilikuwa na vyombo vya habari 1042 vilivyosajiliwa ambapo kati ya hivyo, Magazeti ni 372, Vituo vya Redio 247, Vyombo vya Habari vya Mtandao 355 na Vituo vya Televisheni 68.”

Prof. Kabudi ameongeza kuwa Serikali pia imefanikisha kuanzishwa kwa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari kama inavyoelekezwa na Sheria ya Huduma za Habari Sura ya 229.

“Bodi hii, ambayo ni ya kwanza kuanzishwa tangu kupitishwa kwa sheria hiyo, ilizinduliwa rasmi tarehe 3 Machi, 2025, hili ni fanikio kubwa na la kihistoria katika kulinda na kukuza uhuru, ubora na uwajibikaji katika sekta ya habari nchini Tanzania,” aliongeza Prof. Kabudi.

Aidha, amesema katika kuhakikisha shughuli za Michezo zinafanyika kwa ufanisi, Serikali pia imeanzisha Mfuko wa Maendeleo ya Michezo ambapo jumla ya shilingi bilioni 10.657 zimetolewa.

Prof. Kabudi ameongeza kuwa Serikali imefanikiwa kuhuisha na kuendeleza wazo la muda mrefu la ujenzi wa Sports and Arts Arena, mradi ambao ni wa kisasa na unaotarajiwa kugharimu Shilingi Bilioni 300.

Biashara ya Kaboni kuwanufaisha wananchi - Serikali
Zaidi ya Leseni 100,000 zatolewa na LATRA, njia mpya zaanzishwa