Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), kuanzia mwezi Februari, 2021 hadi mwezi Machi 2025, imetoa leseni 108,658 za usafirishaji, katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), CPA Habibu Suluo ameyasema hayo jijini Dodoma katika kikao kazi na Wahariri, waandishi wa habari na kuongeza kuwa kwa mujibu wa Kifungu cha 5(1)(b) cha Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini, Sura ya 413, LATRA ina wajibu wa kutoa, kuhuisha, kusitisha au kufuta leseni za usafirishaji.
Amesema, leseni za usafirishaji zilizotolewa kwa vyombo vya usafiri wa abiria, mizigo na vyombo vya usafiri wa kukodi ziliongezeka kutoka 226,201 mwaka 2020/21 (Februari, 2021) hadi 334,859 mwaka 2024/25 (Machi, 2025) ikiwa ni ongezeko la leseni 108,658, sawa na asilimia 48.
“Hili ongezeko ni sawa na wastani wa ongezeko la asilimia 12 kila mwaka katika kipindi cha miaka minne. LATRA imeendelea kuboresha usafiri wa umma katika miji na majiji makubwa na imeanzisha njia mpya 1,007 za daladala mkoani Dar es Salaam ili kufika maeneo yasiyofikika na kurefusha baadhi ya njia kwa lengo la kumpunguzia gharama mwananchi,” amesema Suluo.
Aidha, ameongeza kuwa njia za usafiri wa mabasi ya mijini zilizorefushwa kwa upande wa Dar es Salaam ni Mbezi Luis-Kisarawe kupitia barabara ya Malamba Mawili, Banana, Toangoma-Pugu Stesheni kupitia barabara ya Kilwa, Nyerere ikiwemo Kivukoni-Bunju Sokoni kupitia Barabara ya Bagamoyo.
CPA Suluo ametaja njia nyingine kuwa ni Gerezani-Bunju Sokoni kupitia Barabara ya Bagamoyo, Buyuni Sokoni-Stendi Kuu ya Magufuli kupitia Kinyerezi Bunju Sokoni-Stendi Kuu ya Magufuli kupitia Madale,Mbande Kisewe-Gerezani kupitia Barabara ya Kilungule, Chang’ombe, Usalama,Mvuti-Machinga Complex na Tabata Segerea.
Amesema, njia nyingine ni Ngobedi B, Machinga Complex kupitia Nyota Njema, na KitongaGerezani kupitia barabara ya Kilwa, na kwa Arusha mamlaka imefanya mabadiliko ya njia za daladala kwa kuzifanya baadhi ya njia kuwa za mzunguko kwa lengo la kuongeza upatikanaji wa huduma kwenye baadhi ya maeneo ambayo
hayakuwa na huduma.
“Mfano ni njia inayoanzia Kwa Mrombo kupitia Impala, Philips, Sanawari, Chuo cha Ufundi Arusha hadi ‘Fire’ na kurudi kwa Mrombo. Lakini kwa Jiji la Dodoma ambayo ni makao makuu ya nchi,CPA Saluo amesema, zimeanzishwa njia mpya kwa ajili yakuyafikia maeneo mapya ya makazi mapya kutokana na kukua kwa kasi kwa jiji hilo,”
“Mfano wa njia hizo ni Machinga ComplexNjedengwa, Machinga Complex-Mpamaa, Machinga Complex-Chidachi, Machinga Complex-Nzuguni, Machinga Complex-Swaswa na Vyeyula-llazo,” amesema CPA Suluo.
Hata hivyo, amesema hatua ya kuhamishia daladala kituo cha Machinga Complex imesaidia kuwepo kwa njia za mzunguko katikati ya Jiji la Dodoma na hivyo kuongeza upatikanaji wa huduma kwa wananchi, unaoanzia barabara ya Hospitali kupitia Majengo Sokoni hadi Machinga Complex kisha kupitia Uwanja wa Ndege na kurudi mjini.
Mamlaka imekuwa ikiwasajili madereva na baadae kuwapatia vyeti vya kuthibitishwa baada ya kufaulu mtihani wa kuthibitishwa inayofanyika katika Ofisi za LATRA za Mikoa yote 26 Tanzania Bara. Hadi kufikia tarehe 31 Machi, 2025, madereva 33,778 walikuwa wamesajiliwa na taarifa zao kuingizwa kwenye Kanzidata (Database) ya Mamlaka.
Kati ya madereva hawa, madereva 8,172 wamesajiliwa kwenye Mfumo wa Kufuatilia Mwenendo wa Mabasi (VTS) na kupatiwa Kitufe cha Utambuzi wa Dereva (i-button), na madereva 4,563 walifaulu mitihani ya LATRA kati ya 9,191 waliofanya mitihani huo (sawa na ufaulu wa asilimia 49.65) na kupatiwa vyeti vya kuthibitishwa.
Matokeo haya yanaashiria maandalizi hafifu kwa madereva, woga wa mitihani unaofanywa kwa kompyuta, upya wa zoezi la kuthibitisha madereva, na kukosekana kwa utaratibu wa kujisomea/kujiendeleza kwa madereva.