Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amewataka Mawakili wa Serikali kufanya kazi kwa kuzingatia misingi ya kitaaluma na kuhakikisha haki inatendeka miongoni mwa wanajamii.

Dkt. Biteko amesema hayo jijini Dodoma wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Mawakili wa Serikali nchini.

“Ombi langu kwenu Mawakili wa Serikali, fanyeni kazi yenu kwa kuzingatia taaluma yenu ya sheria na kutenda haki, ni wajibu wenu kushauri kwa haki na fanyeni kazi bila kuathiriwa na maslahi ya mnaowashauri wala kuogopa,” amesema Dkt. Biteko

Amesisitiza kwa kuwataka mawakili kufanya kazi ya kuiwezesha Serikali kuwahudumia wananchi kwa kuzingatia misingi ya haki.”Fanyeni kazi ya kutetea Serikali yenu, nendeni mkaishauri Serikali na wakati wote mkatende haki, ifanyeni haki kuwa rafiki yenu na anayetokea mbele yenu aone haki imetendeka hata watakaokuwa wamehukumiwa wakiri wanastahili hukumu waliyopewa.”

Halikadhalika Dkt. Biteko amewapongeza Mawakili wa Serikali  pamoja na wadau mbalimbali kwa kuunda na kuendesha Kamati za Ushauri wa Kisheria za Mikoa na Wilaya pamoja na kuendesha Kliniki za Ushauri wa Kisheria bila malipo katika mikoa mitatu ya Dodoma, Kilimanjaro na Mwanza.

Amesema kuwa Serikali inatambua jitihada zinazofanywa na Asasi za Kiraia, na binafsi katika kuwahudumia wananchi kupata huduma za sheria huku akitaja baadhi ya asasi na vyama hivyo kuwa  ni pamoja na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS)Legal and Human Rights Centre (LHRC), Tanzania Legal Aid Providers (TANLAP), Legal Service Facility (LSF), Tanzania Human Rights Defenders Coalition (THRDC) pamoja na Watoa Huduma za Msaada wa kisheria kama UNDP na UN Women..

Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amemuelekeza Mwanasheria Mkuu wa Serikali kushughulikia changamoto mbalimbali zinazokikabili Chama hicho  cha Mawakili wa Serikali ikiwa ni pamoja na kuwasaidia kupata eneo la kujenga Ofisi za Makuu ya Chama na Vivutio vya Mafunzo kwa Mawakili wa Serikali katika mikoa ya Arusha na Dodoma

Namtumbo kuupokea Mwenge wa uhuru Mei 15, Miradi mbalimbali kuzinduliwa
Wizara imejipanga kutatua kero ya Maji Dodoma jiji - Aweso