Belinda Joseph – Songea.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Songea Michael Mbano, ameonyesha kuridhishwa na namna miradi ya maendeleo inavyotekelezwa katika Manispaa hiyo, akitoa pongezi kwa wataalamu wa halmashauri kwa usimamizi makini unaolenga kuleta mabadiliko kwa jamii.
Akiongoza Kamati ya Fedha na Uongozi ya Halmashauri hiyo, Mbano ameongoza ziara ya ukaguzi wa miradi katika kata nne — Ruhuwiko, Mjimwema, Mjini na Msamala — ambapo miradi mbalimbali inaendelea kutekelezwa kwa kutumia fedha za mapato ya ndani pamoja na michango ya wahisani.
Miongoni mwa miradi iliyokaguliwa ni stendi ya kisasa ya malori inayojengwa eneo la Lilambo kwa gharama ya shilingi milioni 900, shule mpya ya Ruhuwiko (milioni 560 – SEQUIP), na kituo cha afya Subira ambacho kinakamilishwa kwa zaidi ya milioni 115 kutoka mapato ya ndani.
Pia wametembelea duka la dawa katika Kituo cha Afya Mjimwema, ukarabati wa stendi ya bajaji (milioni 38), pamoja na ujenzi wa miundombinu katika Shule ya Sekondari ya Emmanuel Nchimbi unaofadhiliwa na kampuni ya BARRICK (milioni 71.4).
Katika maelezo yake mbele ya wajumbe wa kamati na wataalamu, Meya Mbano alisisitiza kuwa miradi hiyo ni kielelezo cha uwajibikaji wa halmashauri kwa wananchi wake.
“Ni wajibu wetu kuhakikisha kuwa kila senti ya umma inaleta matokeo. Hatuwezi kuruhusu uzembe kwenye miradi inayogusa maisha ya wananchi,” alisema Meya huyo kwa msisitizo.
Aliongeza kuwa mbali na kukamilika kwa wakati, miradi hiyo inapaswa kuwa bora, salama na yenye mazingira safi, ili iweze kutumika kwa ufanisi kwa miaka mingi ijayo.
Kamati hiyo imeahidi kuendelea na utaratibu wa kufuatilia hatua kwa hatua miradi yote inayoendelea kutekelezwa ili kuhakikisha kuwa fedha za umma zinatumika kwa tija na kwa faida ya jamii ya Songea.