Mkurugenzi wa zamani wa Itifaki na Mawasiliano wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), John Mrema, amesema hakuna vikao vya Kamati Kuu na Mkutano Mkuu wa chama hicho viliyoazimia kuzuia uchaguzi.
Mrema ameyasema hayo katika mtandao wake wa X zamani Twitter alipokuwa anamjibu Mwanasheria Mkuu wa chama chao, Dr. Rugemeleza Nshala, baada ya kusisitiza kuwa kinachofanyika wakati huu ukiwemo mkakati wa kususia na kuzuia uchaguzi ni matokeo ya vikao vyao vya Kamati Kuu vya Chadema.
“Nimesoma maoni yako ambayo yamejaa uchungu na maumivu, lawama na kejeli. Umesema kuwa uongozi mpya unasimamia maamuzi ya vikao vya Kamati Kuu na Mkutano Mkuu wa chama, ila hujaweka ushahidi wowote ule kwamba kulikuwa na azimio la KUZUIA UCHAGUZI. Hapakuwa na azimio hilo kama lipo, tafadhali weka ushahidi mezani ili Dunia ijue na iwapuuze wote wenye hoja kinzani”, amesema Mrema.
Kwa siku kadhaa sasa chama hicho kimegubikwa na majibizano kutoka kwa viongozi wa Chadema na makada wao wakiongozwa na Mrema, wanaopinga msimao wa chama chao kususia na kuzuia uchaguzi Mkuu.