Kamati ya Wataalamu wa Masuala ya Habari Zanzibar (ZAMECO) wakiwemo (Klabu ya Waandishi wa Habari Zanzibar (ZPC), Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA -ZNZ), Baraza la Habari Tanzania (MCT), Jumuiya ya Waandishi wa Habari za Maendeleo Zanzibar (WAHAMAZA), pamoja Jukwaa la Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania, Zanzibar wameungana na jamii ya kimataifa kuadhimisha Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani (World Press Freedom Day), ambayo hufanyika Mei 3, kila mwaka.
Kwa Zanzibar kaulimbiu ya mwaka huu inasema, “Sheria nzuri ya Habari ni chachu ya uchaguzi ulio huru na wa haki”, ikilenga kuchochea majadiliano ya kitaifa kuhusu umuhimu wa upatikanaji wa sheria mpya na rafiki yenye kusimamia mazingira salama kwa waandishi wa habari hasa kuelekea kipindi cha uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu.
Taarifa ya ZAMECO iliyotoleea hii leo Mei 3, 2025 imesisitiza maeneo makuu matatu
ambayo ni Sheria Mpya ya Habari Zanzibar, inayozingatia matakwa ya Katiba, Mikataba ya kikanda na kimataifa kuhusu uhuru wa kujieleza.
Aidha sheria hiyo pia inazingatia maoni ya wadau wa habari waliyoyatoa katika mchakato wa uandaaji wa Muswada wa Sheria hiyo, sambamba na hayo Sheria hiyo itasaidia kujenga msingi wa uchaguzi ulio huru, wenye haki na uwazi.
“2. Ulinzi kwa Waandishi wa habari wakati wa uchaguziWaandishi wa habari ni nguzo muhimu ya demokrasia. Wana haki ya kufanya kazi zao bila hofu wala vitisho, mashambulizi au unyanyasaji. ZAMECO inatoa wito kwa vyombo vya dola, vyama vya siasa, na wadau wote kuhakikisha waandishi wa habari wanawekewa ulinzi wa kutosha wakati wakitekeleza majukumu kipindi chote cha uchaguzi na baada,”
“3. Haki ya kuripoti bila kubaguliwa: Vyombo vya habari vina wajibu wa kuwafikia wananchi kwa usawa. ZAMECO inapinga vikali aina zote za ubaguzi kwa misingi ya itikadi, asili ya chombo au mtazamo wa mhariri/mwandishi ikiwamo kuwapo kwa kadi maalum zinazotolewa na Tume ya Uchaguzi, tunashauri kuwa kadi / vitambulisho,
vitolewe kwa kila mwandishi mwenye sifa za kuwa mwandishi na anayetarajia kuripoti wakati wa uchaguzi kwani huo ndio utawala bora, hivyo tunatoa wito kwa Tume ya Uchaguzi, vyombo vya dola na watoa taarifa kuwa wawazi na kutoa ushirikiano kwa vyombo vyote vya habari bila upendeleo,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
ZAMECO pia imetoa wito kwa waandishi wa habari na wadau wengine wa habari
kuendelea kupaza sauti kudai upatikanaji wa Sheria Mpya ya Huduma za Habari
Zanzibar na kuendelea kuwa mabalozi wa uhuru wa habari, uwajibikaji na uwazi katika jamii.