Na Belinda Joseph, Songea – Ruvuma.

Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Ruvuma limewataka watumishi wake kuepuka uadui na wananchi na badala yake kushirikiana nao kwa karibu, kwani jukumu lao kuu ni kuitumikia jamii.

Akizungumza katika bonanza maalum la watumishi wa Jeshi hilo leo Mei 3, 2025, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Zimamoto, Kaimu Kamanda wa Jeshi hilo, Melania Nyabwinyo, aliwahimiza askari kushirikiana kwa karibu na wananchi kwa kuimarisha mahusiano mema na si kujenga uadui.

Akizungumzia kuhusu madai ya wananchi kusema magari ya zimamoto kufika kwenye matukio bila maji, Kamanda Nyabwinyo amekanusha taarifa hizo na kusisitiza kuwa Jeshi hilo hujipanga vyema kwa kuhakikisha linawasilisha vifaa na rasilimali zote muhimu kwa ajili ya kukabiliana na majanga ya moto.

Katika hatua nyingine, Kamanda huyo ametoa pongezi kwa Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji pamoja na Menejimenti yake kwa kuwathamini askari wa Mkoa wa Ruvuma kwa kuwapandisha vyeo, nakuwapongeza askari waliopandishwa kwa kuonyesha bidii kazini na kuwataka waendelee kufanya kazi kwa weledi katika majukumu yao mapya.

Aidha, Kamanda Nyabwinyo amewaalika wananchi wa Ruvuma kushiriki kilele cha maadhimisho ya Wiki ya Zimamoto kitakachofanyika kesho, Mei 4, 2025, katika viwanja vya Stendi ya Mfaranyaki. Alisema tukio hilo litakuwa fursa muhimu kwa jamii kupata elimu sahihi kuhusu huduma za zimamoto na kupata majibu ya maswali yao.

Maadhimisho haya huadhimishwa kimataifa kwa kuwakumbuka askari watano waliopoteza maisha katika moto wa msitu huko Victoria, Australia, pamoja na askari wote waliowahi kupoteza maisha au mali zao katika harakati za kuzima moto, Kamanda amewahimiza askari kuendelea kufanya mazoezi na kuongeza juhudi katika utendaji kazi wa kila siku ili kuongeza ufanisi wa maokozi.

Mradi uchimbaji wa Madini kwa Vijana MBT wazinduliwa
Bukoba: Mvua yaleta maafa familia 18 zikikosa makazi