Belinda Joseph – Songea.

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Ruvuma, Oddo Mwisho, amesema kuwa Chama kitaendelea kumuenzi kwa vitendo Mdau wa Maendeleo Amandius Jordan Tembo, maarufu kama Toronto, kufuatia juhudi zake za kujenga ofisi za CCM katika kata mbili ndani ya Manispaa ya Songea.

Kauli hiyo ameitoa akiwa mgeni rasmi katika hafla ya kukabidhiwa ofisi ya CCM ya Kata ya Bombambili Mei 4, 2025, ofisi iliyojengwa na Toronto Ujenzi wa ofisi hiyo umekamilika kwa kipindi cha miezi mitatu, kama alivyoahidi awali, Mwenyekiti huyo alisema kuwa kukamilika kwa ofisi hiyo kumeongeza hadhi na ari ya kufanya kazi ndani ya Chama.

“Hapa Manispaa ya Songea hatujawahi kushuhudia mdau aliyejitokeza binafsi na kuanzisha ujenzi wa ofisi za CCM. Tunaendelea kumshukuru Toronto kwa moyo wake wa kizalendo,” alisema Mwisho. Aidha, alitoa rai kwa Toronto kusaidia kukamilisha ujenzi wa ofisi zingine ambazo ujenzi wake tayari umeanza katika maeneo mengine ya manispaa hiyo.

Mwenyekiti huyo alimpongeza Toronto kwa kuamua kukijenga chama, na kuongeza kuwa sasa Kata mbili Subira na Bombambili zina ofisi rasmi za kufanyia kazi na vikao vya Chama, jambo linalosaidia kuimarisha utekelezaji wa majukumu.

Aliwataka wadau wengine wa maendeleo kushirikiana na CCM pamoja na serikali katika kusaidia jamii kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwa masilahi mapana ya Taifa.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Bombambili, Jeremiah Milembe, amemshukuru Toronto kwa kuchagua kata hiyo kwa ajili ya ujenzi wa ofisi, na kusema kuwa hatua hiyo itapunguza adha kubwa waliyokuwa wakiipata, ameongeza kuwa utekelezaji wa Ilani ya CCM katika kata hiyo umefikia zaidi ya asilimia 90.

Mdau wa maendeleo, Toronto, ameahidi kuendelea kushirikiana na Chama kuhakikisha kuwa kata nyingine ndani ya Manispaa ya Songea nazo zinajengewa ofisi, amesema kuwa malengo yake ni kuifanya Songea kuwa mji wa mfano kwa maeneo mengine nchini.

Hii ni awamu ya pili kwa Toronto kukamilisha ujenzi wa ofisi za CCM, ambapo awali alijenga katika Kata ya Subira, na sasa katika Kata ya Bombambili. Ujenzi huo umegharimu zaidi ya Shilingi milioni 30, Toronto ameahidi kuanza ujenzi wa ofisi zaidi hivi karibuni ndani ya Wilaya hiyo.

Matukio 74 ya Moto yaripotiwa Kagera Vikoba, uzembe vikihusishwa
Maisha: Aambukizwa ugonjwa wa zinaa kama adhabu