Belinda Joseph, Nyasa – Ruvuma.

Mkuu wa Wilaya ya Nyasa, Peres Magiri ametoa wito kwa wananchi wa wilaya hiyo kujitokeza kwa wingi kushiriki katika mapokezi ya Mwenge wa Uhuru unaotarajiwa kupokelewa Jumatatu, tarehe 12 mwezi huu, katika kijiji cha Ukuli, kata ya Kingerikiti.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Magiri alisema Mwenge wa Uhuru utakagua na kuzindua miradi ya maendeleo iliyoibuliwa na Serikali kwa ushirikiano na wananchi pamoja na wadau wa maendeleo.

“Nawaomba wananchi kushiriki kuanzia mapokezi, kwenye maeneo ya miradi hadi mkesha katika viwanja vya Polisi, Mbambabay,” alisema Magiri.

Aidha, alieleza kuwa maandalizi yanaendelea vizuri, na aliwasihi wote wanaohusika na miradi kuhakikisha wanakamilisha maandalizi mapema. Aliongeza kuwa tukio hilo litachangia kukuza uchumi wa eneo kupitia huduma mbalimbali kama malazi, chakula, usafiri na utalii.

Magiri pia aliwahamasisha wananchi kutoka wilaya za jirani kama Mbinga, Songea na Ludewa kufika kushiriki tukio hilo muhimu, akisema kuwa ni fursa ya kujitangaza kiutalii na kiuchumi.

Kaulimbiu ya mwaka huu ni: “Jitokezeni Kushiriki Uchaguzi Mkuu mwaka 2025 kwa Utulivu na Amani”, ikihimiza mshikamano na uzalendo kuelekea uchaguzi mkuu.

Maisha: Video tata zampotezea kazi Kijana
Nyamguma aibuka mshindi Habari za Nishati Safi ya Kupikia