Belinda Joseph – Ruvuma.
Mwenyekiti wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) Mkoa wa Ruvuma, Wakili Eliseus Ndunguru, amesema kuwa kutokujua sheria hakuwezi kuwa kinga ya kutokuwajibika kisheria, akibainisha kuwa sheria hutungwa na wawakilishi wa wananchi ambao wanaaminika kuwasilisha maoni ya waliowachagua.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Songea katika uhamasishaji wa uelewa wa sheria kwa wananchi, Wakili Ndunguru amesema sheria huanzia ngazi ya familia hadi kimataifa, hivyo ni wajibu wa kila mwananchi kuzifahamu na kuzifuata kwa ajili ya kulinda haki na kutimiza wajibu.
“Wananchi wana jukumu la kulinda haki na kutimiza wajibu wao kwa sababu haki na wajibu vina uhusiano wa moja kwa moja; huwezi kuwa na haki bila kuwa na wajibu, na vyote vinadhibitiwa na sheria,” amesema Ndunguru.

Amesema moja ya changamoto kubwa katika jamii ya Kitanzania ni uelewa mdogo wa wananchi kuhusu sheria, jambo linalosababishwa na ukosefu wa ushirikishwaji katika mchakato wa utungaji wa sheria. Amependekeza kuwa sheria zinapaswa kuanzia ngazi ya chini kwenda juu badala ya kutoka juu kwenda chini.
Wakili Ndunguru amezitaja haki za msingi ambazo kila mwananchi anapaswa kuzifahamu kuwa ni pamoja na haki ya kuishi, haki ya kumiliki mali, uhuru wa kutoa maoni, haki ya kuchagua na kuchaguliwa, pamoja na haki ya kuabudu.
Ametoa wito kwa wananchi kutumia uhuru wa kutoa maoni kwa njia inayozingatia sheria, huku wakiheshimu haki za watu wengine. Ameonya kuwa kutotimiza wajibu wa kufuata sheria kunaweza kupelekea athari kubwa kwa jamii, ikiwemo wananchi kujichukulia sheria mikononi.