Belinda Joseph, Songea – Ruvuma.

Uzalishaji wa zao la tumbaku umeongezeka kutoka tani 1,664 kwa mwaka 2023/2024 hadi kufikia tani 2,053 katika msimu wa mwaka 2024/2025, aidha uzalishaji wa ufuta umefikia tani 5,538 kwa msimu wa mwaka 2024/2025, huku matarajio yakiwa ni kuzalisha tani 10,000 kwa msimu wa mwaka 2025/2026.

Ongezeko hilo limechangiwa na mafanikio ya mfumo wa stakabadhi gharani unaoendelea kuimarika, sambamba na kupanda kwa bei ya mazao ya ufuta, mbaazi na soya, Mafanikio haya yameendelea kuwahamasisha wakulima wengi zaidi kuwekeza kwenye kilimo cha mazao ya biashara.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma, Mary Makondo.

Akizungumza katika Mkutano Mkuu wa 22 wa kawaida wa Chama Kikuu cha Ushirika wa Mazao Songea Namtumbo (SONAMCU) uliofanyika Mei 28, 2025 mjini Songea, Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma, Mary Makondo, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, amesema mkoa unajivunia kuwa na chama kikuu chenye mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa mkoa na Taifa kwa ujumla.

Amesema kuwa SONAMCU kimekuwa mfano wa kuigwa kutokana na kazi nzuri kinayoifanya katika kusimamia uzalishaji na masoko ya mazao ya biashara kama tumbaku, mbaazi, ufuta na soya, amesisitiza kuwa chama hicho kimekuwa kichocheo kikuu cha maendeleo ya wakulima na ushirika mkoani humo.

Aidha, ametumia jukwaa hilo kuwataarifu wananchi kuwa msimu mpya wa minada ya zao la ufuta unatarajiwa kuanza kesho, Mei 29, katika Wilaya ya Namtumbo, amehimiza wakulima kushiriki kikamilifu ili kunufaika na mfumo rasmi wa masoko na kupata bei nzuri ya mazao yao.

Meneja wa SONAMCU Juma Mwanga, amesema kuwa dhamira ya chama hicho ni kusimamia na kuratibu masoko ya mazao ya kibiashara yanayouzwa kupitia mfumo wa stakabadhi gharani, yakiwemo tumbaku, ufuta, mbaazi na soya, amesema kuwa SONAMCU inatoa elimu kwa wakulima kuhusu kilimo bora cha biashara, hali iliyosaidia kuongeza uzalishaji wa mazao hayo.

Meneja wa SONAMCU Juma Mwanga.

Kwa mujibu Mwanga, hatua hizo zimeleta mafanikio makubwa kwa wakulima na kuongeza mapato kwa kaya nyingi zinazotegemea kilimo.

Mdau wa SONAMCU kutoka Wilaya ya Namtumbo, Eleterius Cosmas Mbawala, amesema kuwa hali ya kilimo kwa sasa ni nzuri na wakulima wamefanikiwa kulima na kuvuna kwa mafanikio, meeleza kuwa vyama vya msingi vimekuwa msaada mkubwa kwa wakulima kwa kuwapatia ushauri, pembejeo na usimamizi wa karibu.

Mbawala ameomba Serikali kuangalia uwezekano wa wanunuzi wa mazao kuwalipa kwa kutumia shilingi badala ya dola, akibainisha kuwa wakulima wengi hawana uelewa wa thamani ya dola, jambo linalowapa changamoto katika kufanya maamuzi ya kibiashara.

 

Chama Kikuu cha Ushirika SONAMCU kimeanzishwa mwaka 2003 chini ya Sheria ya Ushirika Na. 15 ya mwaka 1991. Kinaundwa na jumla ya vyama vya msingi 50, ambapo Halmashauri ya Songea ina vyama 7, Manispaa ya Songea vyama 2, Halmashauri ya Madaba chama 1, Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga vyama 3, na Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo vyama 37.

SONAMCU yaombwa kuwasaidia Wakulima wenye changamoto
Serikali yaelekeza nguvu kwenye uchumi wa Wananchi Kata ya Songea mjini