Wakulima wa zao la kahawa katika kijiji cha Mpepo, Wilaya ya Nyasa, mkoani Ruvuma wameishukuru Serikali kwa kuwapatia mbolea ya ruzuku ambayo imeongeza tija na uzalishaji wa zao hilo.
Wamesema kuwa ruzuku hiyo imepunguza gharama za uzalishaji na kuwawezesha kuajiri nguvu kazi zaidi mashambani, tofauti na miaka ya nyuma kabla ya Serikali kuanza kutoa mbolea hiyo.
Ilbert Mahai, mkulima kutoka kijiji cha Mpepo, alisema kuwa baada ya kupata mbolea ya ruzuku, amepunguza gharama alizokuwa akitumia kununua pembejeo kwa ajili ya shamba lake lenye ekari 19. Fedha hizo sasa amezielekeza kulipa vibarua, hivyo kuchangia ajira kwa wakazi wa kijiji hicho na vijiji jirani, hususan vijana na wanawake.
Alisema kuwa tangu aanze kupokea mbolea ya ruzuku, uzalishaji umeongezeka kutoka tani 20 msimu wa 2022/2023 hadi tani 90 msimu wa 2023/2024, na kwa msimu wa 2024/2025 amevuna zaidi ya tani 150.
Aidha, anatarajia mavuno kuongezeka hadi tani 200 msimu wa 2025/2026, kutokana na maandalizi mazuri yaliyowezeshwa na Chama cha Msingi cha Ushirika Mapendo kuwapatia mbegu na pembejeo kwa wakati.
Mahai amewataka vijana wa Nyasa kujikita katika kilimo cha kahawa kwa kuwa kina faida kubwa kiuchumi, huku akitaja kuongezeka kwa bei kutoka Sh. 4,500 kwa kilo msimu wa 2023 hadi Sh. 10,000 msimu wa 2024/2025.
Aidha, ameshauri Serikali kuhakikisha pembejeo zinawafikia wakulima kwa wakati ili kuwawezesha kuandaa mashamba mapema na kuzalisha kahawa bora kwa ajili ya masoko ya ndani na nje ya nchi.
Kwa upande wake, Alto Matembo, mkulima wa kijiji cha Ndondo, alisema kilimo cha kahawa kimemuwezesha kujenga nyumba bora na kusomesha watoto wake hadi vyuo vikuu. Ametoa wito kwa vijana wa kijiji hicho kujiunga na vyama vya msingi vya ushirika (Amcos) ili kupata masoko ya uhakika kupitia vyama hivyo.
Ameiomba Serikali kupitia Wizara ya Kilimo kuendelea kutoa pembejeo za ruzuku kila mwaka na kudhibiti bei zake, ili kupunguza gharama za wakulima kusafiri hadi Wilaya ya Mbinga, umbali wa kilomita 98, ambapo kusafirisha mfuko mmoja wa kilo 50 hugharimu kati ya Sh. 5,000 hadi 6,000.
Naye Method Ngonyani, mkulima wa kijiji cha Mtetema, kata ya Mpepo, ameishukuru Serikali kwa kuanzisha mradi wa kuzalisha miche bora ya kahawa aina ya Kombat. Alisema miche hiyo imehamasisha wakulima wengi kuacha mazao ya kawaida kama mahindi na maharage na kuhamia kahawa yenye faida kubwa.
Ngonyani alisema kuwa miche hiyo inapatikana bure kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa na Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB), hali inayowaondolea usumbufu wa kusafiri hadi Mbinga kununua miche kwa