Belinda Joseph – Songea.

Kituo cha Afya Matimila kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, kimepokea gari jipya la kubebea wagonjwa/Ambulance, lenye thamani ya Shilingi milioni 300 kwa ajili ya kuboresha huduma za rufaa kwa kinamama wajawazito na watoto walio na umri chini ya miaka mitano.

Akizungumza mara baada ya kukabidhi gari hilo kwa Kata ya Matimila, Katibu wa Afya wa Halmashauri hiyo, Nassa Sanga amesema Halmashauri ilipokea rasmi gari hilo kutoka Wizara ya Afya tarehe 26 Mei 2025, amebainisha kuwa ni gari aina ya Land Cruiser Hard Top.

Amewataka wakazi wa kata hiyo kuhakikisha gari hilo linatumika kwa madhumuni yaliyokusudiwa ya kusafirisha wajawazito na watoto kwenda Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Ruvuma.

Sanga ameonya kuwa matumizi mengine yasiyokusudiwa yanaweza kusababisha madhara kwa wananchi, yakiwemo kuchelewa kufikishwa hospitalini kwa ajili ya matibabu ya haraka, huku akisisitiza umuhimu wa gari hilo kutumiwa kwa uangalifu mkubwa ili kuhakikisha linawanufaisha walengwa kwa ufanisi zaidi.

Aidha, ametoa shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, Waziri wa Afya Jenista Mhagama ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Peramiho, pamoja na viongozi wote wa chama na serikali kwa juhudi wanazoendelea kufanya ili kuboresha huduma za afya katika Halmashauri hiyo, hasa katika Kata ya Matimila.

Akikabidhiwa gari hilo kwa niaba ya wananchi, Diwani wa Kata ya Matimila ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Menance Komba, ameahidi kulitunza gari hilo ambalo litasaidia kuokoa maisha ya wananchi na kurahisisha safari za wagonjwa kwenda rufaa, ameeleza kuwa gari hilo litatumika kwa kusafirisha wagonjwa pekee na halitaruhusiwa kubeba bidhaa kama mkaa, mchanga, tofali au kuni.

Kwa upande wake Mzee wa kijiji cha Matimila Elizia Gerald Komba, amesema amefurahishwa na hatua ya serikali kupeleka gari la wagonjwa katika kata hiyo, akieleza kuwa tangu kuzaliwa kwake hajawahi kuona gari la wagonjwa likipelekwa Matimila, amesema wana matumaini kuwa sasa wagonjwa watafikishwa hospitalini kwa wakati.

Naye Agnetha Gerold Nyoni, mkazi wa kata hiyo, amemshukuru Rais Samia, Diwani na Mbunge kwa kufanikisha upatikanaji wa gari hilo amesema awali wanawake walikuwa wakijifungulia njiani kutokana na changamoto ya usafiri, lakini sasa wana imani huduma zitaboreshwa na changamoto hizo kupungua kwa kiasi kikubwa.

Maisha: Mjane alivyoweza kulipa milioni 70 ya mkopo kwa urahisi
Waganga wa Jadi waliojifanya Madaktari Bingwa wadakwa Tanganyika