Serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria imesema kwa mujibu wa kifungu cha 9 cha Sheria ya Ndoa, Sura ya 29, ndoa imetafsiriwa kuwa makubaliano ya hiari kati ya mwanamke na mwanaume kuishi pamoja na inaweza kuwa ya mume mmoja na mke mmoja au mume mmojana wake zaidi ya mmoja.
Akizungumza Leo Bungeni Jijini Dodoma Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Jumanne Sagini wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Noah Sautu ambapo ameuliza Je, lini Serikali italeta marekebisho ya Sheria ya Ndoa kuhusu ndoa ya jinsia moja au Muswada wa Sheria kupiga marufuku ndoa ya jinsia moja.
“Hivyo, Sheria yetu haitambui ndoa ya aina nyingine yoyote isipokuwa kama ilivyotafsiriwa katika Sheria tajwa, Serikali imeendelea kutekeleza mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai ambapo tupo katika hatua za mwisho za kukamilisha Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali za Haki Jinai (The Criminal Justice (Miscellaneous Amendment) Bill)”,
“Ambapo kifungu cha 176 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 kimependekezwa kufanyiwa marekebisho ili kudhibiti vitendo vya ukiukwaji wa maadili ikiwemo vitendo vya ndoa za jinsia moja”. Amesema Sagini
Hata hivyo ameongezea kwa kusema kumekuwepo na ongezeko la ndoa za utotoni hivyo Serikali inaendelea kudhibiti kwa sheria mbalimbali ikiwepo sheria ya mtoto inayozuia Mtoto kufanyiwa vitendo vya uzalilishaji, unyanyasaji pamoja na ndoa za utotoni.