Elimu ya matumizi ya Nishati safi ya kupikia imeendelea kutolewa kwa wananchi wa Wilaya ya Mpanda mkoani Katavi ili kuendana na mabadiliko ya tabia nchi pamoja na utunzaji wa mazingira kwa ajili ya ustawi wa jamii.
Hayo yamebainika katika Tamasha lililopewa jina la ‘Samia Nakuaminia’ lililoandaliwa na Ofisi ya Tarafa ya Misunkumilo,ambalo limelenga kutoa elimu na hamasa kwa umma wa wanakatavi kuhusu masuala ya nishati safi, ushiriki wa wananchi kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025, lishe bora kwa watoto ili kuepuka udumavu, usalama wa kuzingatia wakati wa matumizi ya nishati safi ya kupikia hasa umeme na gesi, ili kuepuka ajali za moto.
Mgeni rasmi katika Tamasha hilo Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Jamila Yusuf amewataka wanachi wa Wilaya hiyo kuendeleza agenda ya utunzaji wa mazingira kwa mustakabali wa Taifa na afya za wananchi hao hasa wakinamama ili kuepukana na uchafuzi wa hali ya hewa na magonjwa mbalimbali.
Afisa Tarafa ya Misunkumilo, Leah Gawaza amesema elimu inayoendelea kutolewa ni mwendelezo wa kuunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan ambaye ni kinara wa mazingira.