Raisi wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmi katika CRDB Bunge Grand Bonanza litakalofanyika siku ya Jumamosi, tarehe 21 Juni, 2025 katika Viwanja vya Shule ya Sekondari John Merlini, iliyopo Miyuji, Jijini Dodoma.
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo Juni 18, 2025, wakati wa makabidhiano ya vifaa kwa ajili ya Bonanza hilo kutoka kwa Wawakilishi wa Benki ya CRDB, Mwenyekiti wa Bunge Bonanza, Festo Sanga amesema Dkt. Samia ni mwana michezo namba moja Nchini na yeye ndiye chanzo cha kuanzishwa kwa Mabonanza ya michezo katika Taasisi mbalimbali.
Amesema Bonanza hilo linalohusisha michezo mbalimbali ya ushidani kati ya Timu za Bunge na Taasisi nyingine za Serikali, pamoja na wadhamini wakuu, lina lengo la kuwahamasisha Wabunge, Watumishi wa Ofisi ya Bunge na Wananchi kwa ujumla kushiriki katika michezo, ili kujenga Afya zao, kutoa burudani na pia kudumisha umoja na kujenga mshikamano miongoni mwao.
Aidha amesema Bonanza hilo limeandaliwa kwa ushirikiano kati ya Benki ya CRDB na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambapo Benki hiyo ndiyo ndiye Mdhamini Mkuu.
Aliongeza kuwa Bonanza hilo litabebwa na kauli Mbiu isemayo “SHIRIKI UCHAGUZI MKUU, KWA MAENDELEO YA TAIFA
LETU”.