Kampuni ya Tanzania Breweries Plc (TBL) kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), Leo wameandaa tukio la kipekee kwa Wakulima wa Mtama lililofanyika Hombolo, Dodoma, likiwakutanisha wakulima, viongozi wa serikali za mitaa, watafiti, taasisi za kifedha na wadau wa maendeleo kwa pamoja wakionesha ubunifu, ushirikiano na mafanikio ya kilimo bora.

Tukio hilo, lililobeba kauli mbiu “Shangwe kwa wakulima!” limelenga kuonyesha uhusiano wa muda mrefu kati ya TBL na wakulima zaidi ya 2,400 walioko katika mpango wa ununuzi wa mtama kwa msimu wa kilimo wa mwaka 2025.

Mpango huo ndio dira kwa manunuzi ya malighafi za ndani ya kampuni . Kwa ujumla, ABINBEV kampuni mama ya TBL inashirikiana na zaidi ya wakulima 20,000 katika mnyororo mzima wa thamani, ambapo zaidi ya asilimia 68 ni wakulima wadogo.

Mpango huu umejikita katika kuwajengea uwezo wakulima kupitia mafunzo, upatikanaji wa takwimu, zana na teknolojia ili kuwasaidia kufanya maamuzi bora. Tunafanya kazi kwa karibu na wakulima kutatua changamoto shambani na kutoa suluhisho kulingana na mazingira yao.

TBL, imekuwa mstari wa mbele katika kuendeleza kilimo endelevu ikiwa na lengo la kuchochea ukuaji jumuishi wa uchumi. Kuongeza tija na faida kwa wakulima kuna matokeo chanya si tu kwenye mnyororo wa thamani bali pia kwenye ustawi wa jamii.

Kwa kushirikiana kuboresha mbinu za kilimo, tunasaidia kuboresha maisha na kuimarisha uchumi wa ndani. Ni muhimu kuwaunga mkono wakulima na jamii zao ili tuendelee kupata malighafi bora na kufurahia bia bora zaidi hapa Tanzania.

Akizungumza wakati wa tukio hilo, Mgeni Rasmi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Mhe. Gerald Mweli alisema, “Ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi kama huu ni muhimu kwa mageuzi ya sekta ya kilimo.

Ushirikiano kati ya TBL, TARI na wakulima wa Hombolo unaonesha jinsi maarifa, teknolojia na uwekezaji vinavyoweza kuleta usalama wa chakula, mafanikio ya kiuchumi, na maendeleo ya taifa.”

Wakati wa hafla hiyo, wakulima walipewa taarifa kuhusu utafiti wa hivi karibuni, teknolojia za kisasa za kilimo na ubunifu unaoungwa mkono na AB InBev, ikiwa ni pamoja na maonesho ya moja kwa moja ya mashine mpya ya kupanda mtama na mbinu bora za upandaji zilizowasilishwa na TARI.

Ubunifu huu unalenga kuongeza tija, kuhimili mabadiliko ya tabia nchi na kutumia ardhi kwa ufanisi zaidi.
Mkurugenzi Mtendaji wa TBL, Bi. Michelle Kilpin, alisema: “Tukio hili linaonesha dhamira yetu ya dhati kwa wakulima wa ndani na kilimo endelevu.

Tunajivunia kuunga mkono ubunifu unaosaidia kuongeza uzalishaji na kubadilisha maisha. Ushirikiano wetu na TARI na msaada endelevu kutoka kampuni mama yetu, AB InBev, unatuwezesha kuendelea kuwekeza kwenye yale yanayowagusa zaidi watu wa jamii zetu.”

Vile vile TBL imetoa mashine za kupandia na kupigia mtama kwa vikundi mbalimbali vya wakulima wa Mtama . Lengo likiwa ni kuzuia upotevu wa mtama wakati wa kuvuna pia kurahisisha shughuli za upandaji wa mtama na kuongeza tija katika uzalishaji.

Siku ya Wakulima wa Mtama pia imeonesha jinsi TBL inavyojipanga kufanikisha Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), hususan:
●SDG 2 – Kutokomeza Njaa: Kwa kuimarisha usalama wa chakula kupitia tija ya kilimo.
●SDG 12 – Matumizi na Uzalishaji Endelevu: Kupitia ununuzi wa mazao endelevu na mbinu bora za kilimo.

●SDG 13 – Hatua Dhidi ya Mabadiliko ya Tabianchi: Kwa kutambulisha teknolojia rafiki kwa mazingira.
●SDG 17 – Ushirikiano kwa Maendeleo: Kupitia ushirikiano wa maana na taasisi kama TARI.

Kwa upande wa TARI, Dkt. Deusdedith Mbazibwa akimuwakilisha Mkurugenzi wa TARI alisema: “Ushirikiano wetu na TBL umejikita katika ubunifu unaotokana na uzoefu wa moja kwa moja mashambani. Kuanzia majaribio ya mbegu hadi kwenye matumizi ya mashine, lengo letu ni kuwawezesha wakulima kwa teknolojia inayotegemea sayansi na inayolenga matokeo.

Tukio la leo linaonesha jinsi teknolojia na mbinu bora za kilimo zinavyoweza kuinua maisha ya vijijini.”

Maadhimisho ya Siku ya Wakulima wa Mtama yamehitimishwa kwa ahadi ya pamoja kutoka kwa wadau wote wa kuendelea kupanua wigo wa elimu ya kilimo na teknolojia ili kuongeza tija, kipato na ustawi wa jamii za wakulima kote nchini.

Lipeni madeni MSD izidi kuboresha huduma - Dkt. Ngaiza
Serikali kufanya mapitio maelekezo ya sheria Sekta ya Ulinzi Binafsi Nchini