Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Hamis Mwenda amefanya ziara katika kiwanda cha Mate Limited kinachozalisha pombe kali (spirit) jijini Dodoma, ambapo amepongeza juhudi za kiwanda hicho katika kuzalisha kwa kiwango cha kitaifa na kuzingatia taratibu za kikodi.
Katika hotuba yake, Kamishna alieleza kuwa lengo la ziara hiyo ni kuhakikisha kuwa wazalishaji wa bidhaa zinazotozwa kodi maalum (excise duty) wanazingatia sheria na kutoa taarifa sahihi za uzalishaji na mauzo.
“Bidhaa kama spirit zinaathari kwa afya na jamii, hivyo ni muhimu ziwe chini ya usimamizi wa karibu. Pia tunataka kuhakikisha kuwa kila kinachozalishwa kinatozwa kodi stahiki kwa mujibu wa sheria,”amesema Kamishna.
Ameeleza kuwa TRA itaendelea kufanya ukaguzi wa kiufundi na kushirikiana na viwanda kwa lengo la kuhakikisha uzingatiaji wa sheria na kuongeza mapato ya ndani ya nchi.
Kwa upande wa, kiongozi wa Mate Limited Adolbert Maimu amemshukuru Kamishna kwa ziara hiyo na kuahidi kuendelea kushirikiana na TRA kwa uwazi na uaminifu, sambamba na kuhakikisha bidhaa zao zinakidhi viwango vya kitaifa.
Ziara hiyo ni sehemu ya mkakati wa TRA wa kufuatilia kwa karibu bidhaa za ushuru wa ziada na kuimarisha mahusiano na sekta binafsi kwa maendeleo ya uchumi wa Taifa.