Kibaha Zoezi la uchukuaji na urejeshaji wa fomu za kugombea nafasi za Ubunge na Udiwani ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Halmashauri ya Mji wa Kibaha Mkoa wa Pwani linaendelea kushika kasi, huku watia nia wakiendelea kujitokeza kuwania nafasi hizo kuelekea Uchaguzi Mkuu ujao.
Leo Juni 30, 2025, Mwalimu Abubakari Alawi amejitokeza tena kuwania nafasi ya Ubunge wa Jimbo la Kibaha Mjini kwa mara ya pili, baada ya kuibuka mshindi wa pili katika mchakato wa mwaka 2020. Akizungumza mara baada ya kurejesha fomu yake, Alawi amesema anaamini muda umefika kwa chama kumpa nafasi ya kulitumikia jimbo hilo akitumia uzoefu na maono aliyoyakusanya kwa muda wote.
Katika upande wa udiwani, Aziza Mruma, aliyekuwa diwani wa Viti Maalum katika Halmashauri ya Mji wa Kibaha, amerejea kuchukua fomu akieleza kuwa anadhamiria kuendelea kuwatumikia wanawake na jamii kwa ujumla, huku akijivunia mafanikio aliyoyapata katika kipindi cha nyuma.
Naye Erick Swai, dereva wa bodaboda maarufu katika Kata ya Picha ya Ndege, amejiunga na orodha ya watia nia kwa kuchukua fomu ya kugombea Udiwani katika kata hiyo. Swai amesema ameamua kugombea kutokana na kiu ya kuleta mabadiliko chanya katika maisha ya vijana, hasa wanaojishughulisha na ajira zisizo rasmi kama bodaboda.
Zoezi la uchukuaji fomu linaendelea katika ofisi za CCM Wilaya ya Kibaha Mjini, huku idadi ya watia nia ikizidi kuongezeka kila uchao.