Afarah suleiman, Hanang’ – Manyara.

Katibu wa Siasa na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Hanang, George Bajuta, leo amejitokeza rasmi kuchukua fomu ya kuwania ubunge wa Jimbo la Hanang kupitia tiketi ya CCM katika uchaguzi mkuu ujao.

Bajuta aliwahi kushiriki pia kura za maoni ndani ya chama hicho katika uchaguzi wa mwaka 2020 na kushika nafasi ya kwanza.

Katika uongozi wake alihudumu kama Mwenyekiti wa Halmashauri ya Hanang kwa kipindi cha miaka mitano, kuanzia mwaka 2015 hadi 2020.

Akizungumza baada ya kuchukua fomu hiyo, Bajuta alisema “Ninajitokeza kwa dhamira ya dhati kuwatumikia wananchi wa Hanang. Uzoefu nilionao, pamoja na ushirikiano wa wanachama wenzangu wa CCM na wananchi kwa ujumla, utanisaidia kutekeleza kwa ufanisi majukumu ya ubunge ikiwa nitapata ridhaa ya chama na wananchi.”

Hatua ya Bajuta kuchukua fomu imezua msisimko miongoni mwa wanachama wa CCM na wakazi wa Hanang, wengi wakimwona kama mgombea mwenye uwezo wa kuleta mabadiliko chanya kutokana na historia yake ya uongozi na usimamizi wa miradi ya maendeleo katika halmashauri hiyo.

Katavi: TRA, Wafanyabiashara washerehekea mafanikio ya makusanyo ya Kodi
Zuhura Mkumba atia nia ubunge Jimbo la Newala Mjini