Na Mwandishi Wetu

Ukisoma mitandaoni na kuona kilichoandikwa na “mashine ya propaganda” ya Chadema kuhusu kesi ya uhaini ya Lissu na kisha ukapata fursa ya kuangalia video halisi za Mahakamani tena kwa jicho la kisheria utabaini kwamba jamii inakosewa pakubwa sana.

Utakachokutana nacho ni headlines za kudanganya sana kama “Lissu Amfokea Wakili wa Serikali, Mtifuano Mkali,” au “Kimewaka Mahakamani, Lissu Ammaliza Wakili wa Serikali,” au “Lissu Atoa Darasa Mahakamani,” n.k.

Leo nitawakelea uchambuzi wa mambo ambayo unapoangalia video za Mahakamani tena kwa jicho la kisheria utabaini masuala muhimu kumhusu Lissu ambayo bahati mbaya umma hauelezwi na hakuna wa kuueleza kwa ufasaha. Yeye na mawakili wake wanaoneshwa kuwa mashujaa wasiostahili!

Kwanza niombe mrejee makala yangu iliyokuwa na anuani ya: “Lissu Anapokuwa Mwanasheria Anayedharau Sheria, Wingi wa Mawakili Hautamsaidia,” ambapo nikieleza makosa ya Lissu kisheria na hulka yake ya kubananga sheria badala ya kuzitii, nilihitimisha kwa ukali kidogo niliposema: “This man is a legal disgrace.”

Haya tuangalie makosa aliyoyafanya leo Lissu alipokuwa akijitetea Mahakamani na akijenga hoja ya “Nolle Prosequi” (Nitarejea kwenye neno hili).

Upole wa Wakili wa Serikali

Labda nianze na hili. Wanachadema wengi katika mitandao yao wanajaribu kujenga picha kuwa mawakili wa serikali wanaoendesha kesi hii wakiongozwa na Wakili Mkuu Mwandamizi Nassoro Katuga sio wabobezi na eti Lissu anawafundisha sheria!

Si kweli, kama mtaalam wa sheria, Wakili Nassoro anayeisimamia Serikali ni mtu mpole lakini makini na nguli wa kutosha tu sana kwenye sheria na hasa sheria za jinai. Msiomjua angalieni rekodi za Mahakama tangu 2010 huyu jamaa anakwenda Mahakama ya Rufaa kupambana na “full bench” katika kesi za jinai.

Lakini ukitaka kumjua zaidi katika nyanja za tafiti na usomi wa masuala ya sheria za jinai mfuatilie katika makala zake alizoandika katika “International Journal of Law, Management and Humanities.”

Ukali na kuhutubia mahakama mda mrefu kama anavyofanya Lissu sio kuwa mbobezi au mdhaifu wa sheria. Sawa ni kipawa lakini sio msingi wa kujua sheria au kushinda kesi.

Ukitaka kujua kuwa Wakili Nassoro hajajaaliwa mbwembwe kama za kina Lissu au Kibatala lakini namuona kuwa mtu mkimya lakini makini kwenye “legal application” na “legal interpretations” angalia mifano michache ya leo alivyomkaanga na kumgaragaza Lissu Mahakamani kwa hoja za upole lakini nzito kisheria (bahati mbaya watanzania hamuambiwi):

Lissu Achemka Achanganya Kesi Mbili Tofauti

Hoja ya kwanza. Hii inaonesha Lissu hana kumbukumbu nzuri pale wakili Nassoro na hata Hakimu walipobidi kusisitiza kwa kumzodoa kuwa kesi anayodai inashahidi alifika mahakamani na akahojiwa sio hii ya uhaini (distinguishable case) na Lissu akakiri kosa hilo ni ishara kuwa mawakili wa serikali hawana mbwembwe ila wako makini. Kwa umakini wao katika hili Lissu akanywea ingawa aling’ang’ana kuendelea kulitungumzia hilo jambo.

Lissu Achemka, Ataja Kesi Isiyohusiana

Pili, Wanasheria wanajua katika rejea za kesi huwezi kutaja kesi ambazo haziendani ama kwa facts, aina ya makosa au hata ngazi ya mahakama.

Leo, ambacho huwezi kuambiwa, Lissu alicite kesi ya Gandhi ya India na kwa mbwembwe akasema kwamba katika kesi hiyo ya uhaini ilisikilizwa kwa kasi ndani ya mwaka mmoja akahoji kwa nini kesi yake inakwenda taratibu? Anateswa kisiasa?

Wakili Nassoro akipangua hoja hiyo ya Lissu kwanza alitumia tu elimu ya first year kwenye “legal method” alipomuumbua Lissu kuwa kisheria kesi aliyoitaja (akataja hado ukurasa) haifanani na iliyopo sasa hivyo kisheria haiwezi kutumika kama rejea (precedent).

Wakili Nassoro alibainisha kuwa wakati kesi ya Gandhi ilikuwa hatua ya kusikilizwa kwenye Mahakama Kuu, hii ya sasa ya Lissu iko hatua za awali (committal proccedings) Mahakama ya Hakimu Mkazi kabla haijawasilishwa Mahakama Kuu kwa ajili ya kusikilizwa (trial proceedings).

Hatua mbili tofauti kisheria hivyo ni tofauti (distinguishable). Jambo hili mwanafunzi wa mwaka wa kwanza tu darasa la sheria hufundishwa

Lissu Azodolewa kwa kuleta siasa kwenye sheria

Tatu, Ukitaka kumjua Wakili Nassoro, nasisitiza tena, ni mpole ila makini kwenye sheria, ni pale Lissu aliponukuu vifungu kadhaa kwenye Sheria ya Vyama vya siasa ikiwemo kifungu cha 19 alipojaribu kujenga hoja tata kuwa Chama chake kinapaswa au kinahaki ya kushiriki siasa hivyo kuswekwa kwake ndani ni kama anazuiwa kufanya masuala yake ya kisiasa na akaenda mbali kusema Msajili hawezi kukifuza Chama hicho!

Kwanza ama Lissu amesahau au vipi hoja hii imeibua utata mitandaoni kuwa Je, /alikiwa anamaanisha kuwa Chadema wako tayari sasa kushiriki uchaguzi waliousema kuwa hawautaki? Imeacha gumzo!

Lakini nikiri kuwa akijibu hoja hiyo Wakili Nassoro alinifurahisha sana slipoiomba mahakama iachane na hoja hiyo ya Lissu maana haieleweki na haielezeki jinsi ilivyokuwa nje ya msingi wa kesi iliyoko mezani.

Akaenda kifungu cha 39A kinachounda kosa la jinai akasema: “Hakuna sheria inayosema mwaka huu ni wa uchaguzi hivyo mwanasiasa ukifanya kosa uachwe. Hakuna sheria hiyo na bahati nzuri naye (mshtakiwa yaani Lissu) hakuitaja,” aliumbua Wakili wa Serikali.

Lissu Atia Aibu, Akosea Vifungu, Wakili wa Serikali Ampa Somo!

Headlines kama hizi huwezi kuzisikia kutokea mahakamani. Ni bahati mbaya sana. Hata hivyo leo Lissu ametia aibu alipokuwa akijenga hoja kuhusu kutaka kesi yake ifutwe kwa DPP kuleta nia ya kutotaka kuendelea nayo (Nolle Proseque) lakini akataja kifungu cha 245 ambacho kilibadilishwa na sheria ila Lissu akawa hajui!

Kwa upole wake lakini kwa umakini na akitoa shule kubwa Wakili Nassoro wa upande wa Serikali akamuomba Hakimu aachane na hoja hiyo ya Lissu kwani imejengwa katika msingi wa kifungu cha sheria ambacho hakipo.

Kuona Lissu anababaika na anazidi kupotezwa na wakili wa Serikali, mmoja wa mawakili wake akaomba ruhusa ya Mahakama (leave of the Court) amnong’oneze jambo. Lissu akakataa na kujiona yupo powa!

Hakimu akiona Lissu “anaingia chaka” kwa lugha ya mtaani, mara mbili akamuelekeza Lissu akubali kunong’onezwa ndipo akakubali.

Lahaula mike zikawa on, wakili wa Lissu akasikika akimweleza Lissu kuwa amekosea kutaja kifungu, mwanasheria wa Serikali yuko sahihi kifungu ni cha 262 na sio 245, Lissu akabaki kung’aka!!

Ndio maana narudia tena iwe waandishi au mashine ya propaganda ya Chadema ndio wanaofanya wanayoyasambaza mitandaoni, umma kuna mengi hauelezwi kuhusu yanayojiri kesi ya Lissu.

Kuna mengi lakini andelea kupata ya upande wa pili wa kesi hii kwa kuendelea kufuatilia makala haya kujua mengi ambayo wengine hawatakujuza!!

Mwandishi ni Wakili wa Mahakama Kuu na mchambuzi wa masuala ya sheria na katiba.

Tamasha la SAMIA DAY kutikisa Katavi Julai 4
Maisha: Hili hapa suluhisho kwa Wanawake wanaosumbuka kupata watoto