Swaum Katambo – Tanganyika.
Manoni Mbisi ni mlemavu wa macho mkazi wa kijiji cha Bulamata wilayani Tanganyika mkoani Katavi ni mmoja kati ya wanufaika wa mkopo wa asilimia 10 unaotolewa na Halmshauri, ambaye amejitokeza kuchukua mkopo wa shilingi milioni mbili ambao anaamini utamsaidia katika kukuza biashara yake ya mazao na kuachana kabisa na kazi ya kuomba omba mtaani.
Mbisi amesema baada ya kupokea mkopo huo atakuwa balozi mzuri kwa walemavu wenzake na kuwahamasisha kuachana na kazi ya ombaomba na badala yake kujitokeza kuomba mikopo inayotolewa na Halmshauri ili kufanya shughuli zitakazowawezeha kujikwamua kiuchumi.
Katika hafla ya utoaji wa mikopo ya sh 525,058,000 kwa vikundi 51 vya wanawake,vikundi vya vijana 48 na watu wenye ulemavu 7 baadhi yao wamewaomba wakinababa wanaozuia wake zao kujiunga katika vikundi mbalimbali kuacha tabia hiyo huku wengine wakiomba wanawake wenzao kuacha viburi kwa waume zao pindi wanapopokea mikopo hiyo.
Kwa upande wake Afisa Maendeleo Halmshauri ya Wilaya ya Tanganyika Halima Kitumba amesema wametoa mikopo hiyo kwa vikundi 106 na hivyo wanampango kabambe wa kuhakikisha wanufaika hao wanarejesha fedha hizo kwa wakati.
Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika Onesmo Buswelu ambaye ni mgeni rasmi kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Katavi katika hafla hiyo amewataka wanufaika hao kutochukulia mikopo hiyo kama fedha za sadaka na badala yake kufanya biashara zilizokusudiwa.
DC Busweku ameagiza Halmashauri kuwapatia elimu ya kitaalamu wanufaika wa mikopo hiyo ili waweze kujikwamua kimaisha kwa kuwa wanufaika hao licha ya kupata fedha hizo, wengi wao wanakosa elimu na ujuzi wa kuendeleza na kuzalisha fedha hizo, ili waweze kulipa marejesho yao kwa wakati.