Swaum Katambo, Katavi.
Kufuatia ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyofanya mwaka jana mkoani Katavi na kutangaza kufanya filamu ya Royal Tour ambayo ni ombi kutoka kwa Waziri Mkuu Mstaafu Mizengo Pinda,timu Kizimkazi Vijana wa De Jong kutoka visiwani Zanzibar imewasili mkoani Katavi kwa ziara maalum ya kutembelea vivutio vya asili, ikiwa ni sehemu ya ushiriki wao katika tamasha kubwa la ‘Samia Day’.
Mara baada ya kuwasili, vijana hao walipata fursa ya kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Katavi, mojawapo ya hifadhi zinazojivunia mandhari ya kuvutia, wanyama pori adimu na utajiri mkubwa wa maliasili.
Tamasha la ‘Samia Day’ limebeba dhima ya kuonesha mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, huku likitangaza vivutio vya utalii na uwekezaji vilivyopo mkoani Katavi.
Mbali na hifadhi, Timu Kizimkazi pia ilitembelea baadhi ya miradi mikubwa ya kimkakati inayotekelezwa mkoani humo, ikiwemo Mradi wa Maji wa Miji 28 katika Kata ya Shanwe, maghala ya kuhifadhia mazao ya NFRA, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Katavi, pamoja na kituo cha kupozea umeme wa Gridi ya Taifa.
Ziara hiyo imelenga kuwa sehemu ya hamasa kwa vijana kushiriki katika kutangaza utalii wa ndani na kufahamu miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwa manufaa ya Watanzania wote.