SHIRIKA la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limefanikiwa kupeleka mawasiliano kwenye mikoa yote 26 ya Tanzania pamoja na wilaya zake, kupitia Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano. Jumla ya wilaya 112 kati ya Wilaya 139, zimefanikiwa kupata huduma bora na za uhakika za mawasiliano huku zikisalia wilaya 27 kuweza kuunganisha zote nchini.

Akizungumza leo ndani ya Banda la TTCL, kwenye Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara – Sabasaba, Mhandisi Mwandamizi Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, BW. Rishiandumi Jeremia amesema kufikia mwezi wa 12 mwaka huu (2025) wilaya zote zitakuwa zimeunganishwa na mkongo wa Mawasiliano wa taifa.

“Mpaka sasa tayari tumefika katika mikoa yote ya Tanzania Bara, tumeweza kuunganisha jumla ya wilaya 112 za Tanzania kati ya wilaya 139, kwa hiyo tumebakiza wilaya 27 ambazo tuko kwenye ujenzi tunategemea mpaka kufikia mwezi wa 12 mwaka huu kuwa tumekamilisha kuunganisha wilaya zilizosalia,” alisema Mhandisi Jeremia.

Kwa upande mwingine tumefanikia kuunga nchi jirani ambazo tunafanya huduma hiyo kibiasdhara, mfano kwa nchi ya Kenya tumeiunganisha kupitia njia tatu yaani mpaka wa Horohoro, Namanga na Sirari; huku nchi zingine zinazohudumiwa na mkongo wa Taifa ni pamoja na Uganda, Rwanda, Burundi, Malawi, Zambia na Mozambiki. Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano upo kwenye mchakato wa kuziunga pia nchi ya Kongo DRC, ambapo hadi kufikia mwezi wa 12 itakuwa imeunganishwa.

Mkongo wa taifa ni njia ya mawasiliano, ambao umejengwa na Serikali kwa nia ya kupeleka mawasiliano katika mikoa yote ya Tanzania na wilaya zake zote, lakini pia pamoja na nchi za jirani na Tanzania. Ni mtandao wa mawasiliano ya ndani pamoja na nchi jirani zinazotuzunguka.

Kwa upande mwingine, TTCL imefanikiwa kusambaza huduma ya intaneti kupitia faiba mlangoni kwako kwa idadi kubwa ya wananchi wahitaji katika mikoa mbalimbali na inaendelea, huku ikiendelea kuwafungia wananchi kadri wanavyoomba hivyo kuwataka wanaopenda huduma hivyo kuwasiliana na ofisi za TTCL zilizopo karibu nao ili kupewa utaratibu.

Alisema maitaji ya huduma za intaneti kwa sasa ni makubwa hasa ukizingatia mapinduzi makubwa ya uchumi wa kidijitali, jambo ambalo linalochochea jamii kutegemea huduma hiyo kwa kiwango kikubwa, hivyo TTCL lazima iendelee kuwajengea wananchi upatiokanaji wa huduma za uhakiza za intaneti popote, yaani majumbani na maofisini.

Naye Afisa Huduma kwa Wateja (Mauzo) TTCL, Bw. Francis Lubinga amesema taasisi hiyo kwa sasa inaendelea kufunga huduma za intaneti za umma ‘Public Wi-fi’ maeneo mbalimbali ili kufikisha huduma hiyo popote kwa wananchi.

“…Huduma hii unaweza kuiita mtandao usiotumia waya kwa umma, Tumejitahidi kusambaza huduma hii maeneo mbalimbali ikiwemo sekta ya afya, Sekta ya elimu na pamoja na sekta ya utalii ili kuchochera utalii wa nchi yetu na kuutangaza pia ulimwenguni.

Aliongeza kuwa sekta ya utalii wamefunga huduma ya public wi-fi katika vituo vyote vya Mlima Kilimanjaro kupitia njia ya Marangu, ambapo kwa sasa wapandaji wanauwezo wa kupata mtandao wa intaneti hadi katika kilele cha mlima huo huku wakiwa wenapanda.

“Tumefunga pia huduma hiyo katika sekta ya afya kwa Hospitali ya Muhimbili na tunaendelea kufunga katika hospitali mbalimbali ili wananchi waendelee kufurahiya huduma ya inaneti popote hata kama wapo katika hospitali zetu wakipata huduma,” alisema Lubinga.

Sekta ya Kilimo ina mchango mkubwa katika Pato la Taifa - Dkt. Biteko
Timu Kizimkazi yatembelea Hifadhi ya Taifa Katavi