Takriban watu 30 wamekufa maji na wengine 167 hawajulikani walipo baada ya Boti waliyokuwa wakisafiria kupinduka Mto Kongouliopo kaskazini magharibi mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo – DRC.
Waziri wa Afya Jimbo la Equateur, Didier Mbula amesema katika ajali hiyo iliyotokkea hapo jana Oktoba 15, 2023 jumla ya watu 189 waliokolewa na shughuli za kuwatafuta manusura wengine zinaendelea.
Amesema, “hadi sasa kama Serikali ya jimbo tumeopoa maiti 30 na watu 167 hawajapatikana, lakini ajali mbaya za boti hutokea mara kwa mara katika mito na maziwa ya hapa Kongo, hii husababishwa na boti hizi ambazo mara nyingi hupakiwa kupita kiasi.”
Nchi hiyo ina barabara chache za lami katika eneo lake kubwa lenye misitu, na kusafiri kupitia mito ni jambo la kawaida ambapo inaarifiwa kuwa Boti hiyo iliyotengenezwa kienyeji ambayo ilipinduka karibu na mji wa Mbandaka, ilikuwa imejaa kupita kiasi, ikiwa imebeba zaidi ya watu 300, na ilikuwa ikisafiri usiku.