Polisi nchini Kenya, hii leo Julai 25, 2022 imesema idadi ya waliofariki katika ajali ya basi la Morden Coast iliyotokea katika daraja moja katikati mwa nchi hiyo imeongezeka hadi kufikia watu 30.
Ajali hiyo ilitokana na Basi la abiria lililokuwa limebeba idadi ya watu isiyojulikana jana jioni ya Jumapili Juni 24, 2022 kuanguka kwenye daraja na kutumbukia mtoni kando kando ya barabara kuu ya kutoka Meru kuelekea mji mkuu, Nairobi.
Afisa Mkuu wa Polisi jijini Nairobi, Rono Bunei amesema, “Basi hilo lazima lilipata hitilafu ya breki, kwa sababu lilikuwa katika mwendo wa kasi wakati ajali hiyo ilipotokea na kusababisha watu wengi kupoteza maisha.”
Bunei, ambaye alikuwa akiongea na vyombo vya Habari, kupitia taarifa yake amesema, idadi ya waliofariki iliongezeka kutoka watu 24 waliotangazwa usiku na kufikia watu hao 30 ambapo amedai kuwa bado majeruhi wengine wamelazwa Hospitalini.
Ajali hiyo, ni mfululizo wa ajali mbaya kuwahi kutokea nchini Kenya na katika eneo zima la Afrika Mashariki ambako inadaiwa maeneo mengi barabara ni nyembamba, huku Polisi ikiwalaumu madereva wanaoendesha kwa kasi na kusababisha ajali.
Julai 8, 2022 abiria wengine 20 walifariki katika ajali iliyotokea kwenye barabara kuu ya kutoka Nairobi kuelekea mji wa pwani wa Mombasa.