Kocha Mkuu wa muda wa timu ya taifa ya Uganda ‘The Cranes’, Abdallah Mubiru leo Ijumaa (Machi 05) ametangaza kikosi cha wachezaji wa awali thelathini na moja (31) kuelekea kwenye michezo ya kufuzu Fainali za Mataifa Barani Afrika (AFCON 2022).
Kocha Mubiru alitangaza kikosi hicho kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika makao makuu ya Shirikisho “FUFA” mjini Mengo.
Katika kikosi cha wachezaji 31 kilichotajwa na kocha huyo mzaliwa Uganda, wachezaji saba (7) pekee wanacheza ligi ya soka nchini humo na ishirini na nne (24) wanacheza Soka la kulipwa katika mataifa mbalimbali.
Wachezaji wa wanaocheza katika Ligi Kuu ya Uganda ni nahodha wa KCCA FC, Charles Lukwago, nahodha wa Vipers SC, Halid Lwaliwa, Beki wa Express FC, Murushid Juuko, Gavin Mugweri Kizito kutoka SC Villa, Bobosi Byaruhanga wa Vipers SC, Yunus Ssentamu na Ibrahim Oriti (Vipers SC).
Katika Orodha hiyo, wachezaji wanaocheza Ligi Kuu ya Tanzania Bara wapo watatu ambao ni kipa wa Azam FC, Kigonya Mathias ambaye atakuwa na kazi mbele ya Dennis Onyango wa Mamelodi Sundowns, Jamal Salim wa Al Hilal SC na Charles Lukwago wa KCCA FC.
Pia yupo wa Azam FC, Nicolas Wakiro Wadada Ambaye ni miongoni mwa mabeki 10 kwenye kikosi sambamba na kiungo wa Simba SC, Lwanga Taddeo akiwa miongoni mwa viungo 11.
Uganda itakuwa mwenyeji wa Burkina Faso mjini Kampala Machi 24 kabla ya kusafiri kwenda Malawi kwa mchezo wa tarehe Machi 29.
The Cranes inashika nafasi ya pili ikiwa na alama saba, moja nyuma ya vinara wa Kundi B, Burkina Faso, wakifuatiwa na Malawi, huku Sudan Kusini wakiburuza mkia.