Raia 32 wa Kenya wamehukumiwa vifungo vya miaka 20 jela kwa kila mmoja na Mahakama ya kijeshi nchini Uganda kwa kupatikana na silaha kinyume na sheria.
Kupitia kikao cha Mahakama kanda ya Karamoja kaskazini mashakiriki mwa nchi hiyo, ilitolewa adhabu hiyo kutokana na hatia ya wafugaji hao wa jamii ya Turkana kupatikana silaha aina ya bunduki na risasi.
Kundi hilo ni miongoni mwa washukiwa waliokamatwa Aprili 8, 2023 katika maficho yao wakiwa na bunduki 31 na risasi 751katika operesheni inayoendelea ya kukamata silaha zinazomilikiwa kinyume na sheria.
Awali, watu wa jamii ya Karamoja walikuwa wamewasilisha malalamiko kuhusiana na kucheleweshwa kwa kesi hiyo, kwani mshukiwa anapaswa kufikishwa mahakamani katika muda wa saa 48 baada ya kukamatwa.
Jamii za wafugaji wanaohamahama eneo hilo ambalo ni makutano ya mataifa manne ya Sudan kusini, Ethiopia, Kenya na Uganda, zina uhuru wa kuvuka mipaka na kuingia nchi jirani iwapo kuna uhaba wa malisho nchini kwao.