Wanachama 400 na aliyekuwa Diwani wa kata ya Bagara na Mwenyekiti wa kitongoji cha Ngarenaro Mjini Babati mkoani Manyara, Nicodemus Tlaghasi ( Chadema), waliojiuzulu hivi karibuni wamekabidhiwa kadi za CCM.
Katibu Uenezi, siasa, Uhusiano na kimataifa Kanali Mstaafu Ngemela Lubinga amekabidhi kadi za CCM kwa wanachama hao wapya na diwani huyo aliyejiuzulu jana mjini Babati.
Lubinga amewataka wanachama hao 400 na Tglaghasi, kuwa waaminifu kwenye chama hicho.
”Inapotajwa CCM mpya na Tanzania mpya maana yake ni kuwa Watanzania wa sasa mahitaji yao si ya juzi na jana hivyo viongozi waliopatiwa dhamana ya kuongeza inawabidi watimize wajibu wao ipasavyo” amesema Lubinga.
Tlaghasi amesema amechoka kuishi maisha ya wasiwasi yasiyo na amani ambayo alikuwa anayaishi wakati akiwa kiongozi wa jamii kupitia Chadema.
Amesema alikuwa anaishi maisha ya kuvizia ili aonekane na viongozi wa Chadema pindi akitaka kutimiziwa mahitaji ya jamii kwenye Serikali kwani alikuwa anaonekana kama msaliti.
”Ili kuonana na kiongozi wa serikali ilinipasa kuvizia, lengo likiwa nitimize mahitaji ya wapiga kura wangu, nikajiuliza nataseka hivi kwa ajili ya nini? alihoji Tlaghasi.
Amesema dhamira yake ikamtuma kuachana na Chadema na kujiunga na CCM ili aungane na Rais John Pombe Magufuli na Mkuu wa mkoa wa huo Alexander Mnyeti katika kuwatumikia wananchi.