Takriban watu 50 wanadaiwa kufariki dunia baada ya kuangukiwa na kifusi cha udongo katika mgodi wa dhahabu karibu na eneo la Kamituga mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
“Wachimbaji kadhaa walikuwa kwenye kisima ambacho kilifunikwa na udongo na hakuna mtu aliyeweza kuokolewa, inadaiwa kuwa vijana hamsini ndio walikuwa katika shimo hilo la mgodi,” amesema Emiliane Itongwa, kiongozi wa shirika moja la wanawake nchini humo.
Mikasa kama hii hutokea mara nyingi katika nchi mbalimbali duniani, na watu wamekuwa wakipoteza maisha kutokana na hali hiyo.
Licha ya DRC kuwa ni nchi tajiri kwa dhahabu, almasi na coltan lakini migodi mingi inadhibitiwa na makundi yenye silaha na watu wa DRC ni miongoni mwa watu maskini zaidi barani Afrika.
Mashariki mwa DRC kumekuwa na migogoro kwa karibu miaka 24 sasa, huku wote jeshi na makundi ya waasi yakituhumiwa kutumia mapigano kama kisingizio wakati vikichota utajiri wa madini katika eneo hilo.
Mei 2011, serikali ya DRC iliondoa kizuizi kwenye machimbo ya mashariki, eneo lililoathiriwa zaidi na migogoro ya DRC kwa muda mrefu.