Watu 50,000 wametia sahihi pingamizi dhidi ya kampuni ya kimarekani ya Disney kutumia maneno ya Kiswahili ‘Hakuna Matata’ kama utambulisho wa kibiashara.
Sahihi za pingamizi hilo zimekusanywa mtandaoni na mwanaharakati maarufu wa Zimbabwe, Shelton Mpala. Mwanaharakati huyo ameiambia CNN kuwa lengo la kampeni hiyo kulinda utamaduni wa Kiafrika, utambulisho wake pamoja na urithi wa bara hilo kutotumika kuwaneemesha kibiashara watu wa mbali.
“Maneno haya yanayotumika ambayo ni urithi wa bara letu yamegeuka kuwaneemesha kifedha makampuni ya dunia ya kwanza na hata majumba ya historia yaliyoko huko badala ya asili ya watu walioyatengeneza, kuyatunga au kuwafikisha kwenye dunia,” alisema Mpala.
Neno ‘Hakuna Matata’ ambalo linatumiwa sana katika maeneo ya Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika, lilipata umaarufu zaidi duniani baada ya kutumika kwenye wimbo wa filamu ya ‘The Lion King’ ya Kampuni ya Disney mwaka 1994.
Aidha, kumbukumbu za Ofisi inayoshughulikia utambuzi wa biashara nchini Marekani zinaonesha kuwa mwaka huohuo, Disney waliamua kusajili neno hilo kama utambulisho wao wa kibiashara (trademark).
Hata hivyo, mtaalam wa masuala ya sheria za haki miliki kutoka Kenya, Liz Lenjo amepinga uamuzi wa mwanaharati huyo akieleza kuwa hakuna haki iliyoibwa kwa matumizi ya neno hilo kama biashara.
“Hatua ya Disney kutumia ‘Hakuna Matata’ hakukwapua thamani ya lugha yetu adhimu ya Kiswahili. Hii ni kwa sababu mtu yeyote anayezungumza Kiswahili duniani kote hajakatazwa kutumia neno hilo kwa namna yeyote,” alisema Lenjo.
Kampuni ya Disney ambayo inajulikana kwa urefu kama The Walt Disney yenye makao yake makuu California nchini Marekani, inajishughulisha na uandaaji wa maudhui ya televisheni hususan burudani za aina mbalimbali ikiwa ni pamoja na vipindi vya katuni za watoto. Kampuni hiyo haijasema lolote kuhusu ukusanywaji wa saini dhidi yake.