Wachezaji kutoka England  Kyle Walker, Kieran Trippier na Harry Kane wametajwa kwenye orodha ya wanaowania kuingia kwenye kikosi cha wachezaji 11 bora wa FIFA (Fifpro World XI), sambamba na wachezaji saba wa mabingwa wa soka duniani timu ya taifa ya Ufaransa.

Mshambuliaji kutoka England na klabu ya Tottenham Harry Kane ameingia katika orodha hiyo, baada ya kutwaa kiatu cha dhahabu kufuatia kuwa mfungaji bora wa ligi wa Premier msimu uliopita, pamoja na kutoa mchango kwa timu yake ya taifa hadi kufika hatua ya nusu fainali ya kombe la dunia nchini Urusi.

Wachezaji kutoka Ufaransa Antoine Griezmann, N’Golo Kante, Kylian Mbappe, Benjamin Pavard, Paul Pogba, Samuel Umtiti na Raphael Varane, wanabebwa na sifa ya kufanikisha lengo la kutwaa ubingwa wa dunia, mwezi Julai nchini Urusi.

Katika orodha hiyo iliyotolewa na FIFA, klabu ya Liverpool imetoa wachezaji wanne ambao ni Sadio Mane, Mohammed Salah, Virgil van Dijk na Dejan Lovren ambao wametajwa kwa mara ya kwanza.

Mshambuliaji wa klabu bingwa barani Ulaya Real Madrid na timu ya taifa ya Wales Gareth Bale ameachwa, huku kukiwa hakuna mchezaji yoyote kutoka nchi za Scottish ama Ireland ya kaskazini.

Orodha hiyo itapigiwa kura na wachezaji wa soka 25,000 kutoka katika mataifa 65 duniani.

Wapiga kura wote wataruhusiwa kuchagua mlinda mlango mmoja, mabeki wanne, viungo watatu na washambuliaji watatu, ili kutengeneza kikosi bora cha FIFA kwa msimu wa 2017-18.

Orodha ya mwisho ya wachezaji bora 11 wa FIFA, itatangazwa kwenye hafla za utoaji wa tuzo ya shirikisho hilo, ambayo itafanyika jijini London Septemba 24.

Orodha ya wachezaji 55 iliyotolewa na FIFA.

Makipa: Gianluigi Buffon, Thibaut Courtois, David de Gea, Keylor Navas na Marc-Andre ter Stegen.

Mabeki: Jordi Alba, Dani Alves, Daniel Carvajal, Giorgio Chiellini, Virgil van Dijk, Diego Godin, Mats Hummels, Joshua Kimmich, Dejan Lovren, Marcelo, Yerry Mina, Benjamin Pavard, Gerard Pique, Sergio Ramos, Thiago Silva, Kieran Trippier, Samuel Umtiti, Raphael Varane, Sime Vrsaljko na Kyle Walker.

Viungo: Sergio Busquets, Casemiro, Philippe Coutinho, Kevin De Bruyne, Eden Hazard, Andres Iniesta, Isco, N’Golo Kante, Toni Kroos, Nemanja Matic, Luka Modric, Paul Pogba, Ivan Rakitic, David Silva na Arturo Vidal.

Washambuliaji: Karim Benzema, Edinson Cavani, Paulo Dybala, Antoine Griezmann, Harry Kane, Robert Lewandowski, Romelu Lukaku, Mario Mandzukic, Sadio Mane, Kylian Mbappe, Lionel Messi, Neymar, Cristiano Ronaldo na Mohammed Salah.

 

Bashe amkingia kifua mgombea Ubunge wa Chadema
Habari kubwa katika Magazeti ya Tanzania leo Septemba 11, 2018