Jeshi la polisi mkoani Dodoma linawashikilia wahalifu saba kwa tuhuma tofauti tofauti mara baada ya kufanya msako na doria katika maeneo ya Manispaa ya Dodoma na mji mdogo wa Kibaigwa wilayani Kongwa.
Taarifa hiyo imethibitishwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto ambaye amesema kupitia doria hiyo wamemkamata mfanyabiashara mkazi wa Nkuhungu Manispaa ya Dodoma, Josephat Komba (28) akiwa na pikipiki tano aina ya boxer ambazo ni za wizi.
Amewaomba wananchi wa mkoa Dodoma ambao wamepotelewa pikipiki waende kuzitambua.
Pia wamemkamata Mkazi wa Chang’ombe, manispaa ya Dodoma, Nassoro Masangu (27) aliyetafutwa muda mrefu akidaiwa kuvunja nyumba za watu usiku na kubaka wanawake.
Jeshi hilo pia limekamata watuhumiwa wengine watano kwa unyang’anyi kwa kutumia pikipiki kupora na kutoroka baada ya kufanya matukio hayo. Wamekamatwa wakiwa na pikipiki tatu.
Watuhumiwa hao ni Idd Yusufu (22) mkazi wa Chinangali, Ramadhani Juma (21) wa Hazina, Maneno Jonas (20) wa Chang’ombe, Mohamed Mbinga (22) wa Chinangali na Nzoyi Peter (24) wa Nkuhungu.