Serikali ya Liberia imetangaza kuingia hasara kubwa baada ya watu wasio waaminifu nchini humo kuiba asilimia 60 ya umeme wote unaosambazwa, wakijiunganishia kwa wizi kwenye nyumba na biashara zao.

Shirika la umeme nchini humo limeeleza kupitia kipindi cha radio kuwa limekuwa likiingia hasara ya hadi $35 milioni kila mwaka kutokana na wizi huo. Shirika hilo limeeleza kuwa hali hiyo ni uporaji wa mali na fedha za umma unaofanywa na wananchi wasio waaminifu.

Liberia iko katika mkakati wa kuhakikisha inaunda upya sekta ya nishati ambayo ilihujumiwa kwa kiwango kikubwa wakati wa vita ya wenyewe kwa wenyewe kati ya mwaka 1989 na 2003.

Imeelezwa kuwa wizi wa umeme ukithiri nchini humo sio kwa sababu ya umasikini, bali ni kwa sababu watu wengi hawajafikishiwa umeme hivyo waonapo nyaya za umeme zinapita karibu na maeneo yao hujiunganishia kinyamela ili wao pia wapate umeme.

Marekani imeendelea kutoa msaada wa kiufundi na kifedha kwa taifa hilo la Afrika Magharibi kwa lengo la kuongeza idadi ya kaya zilizounganishiwa umeme kama sehemu ya mpango mkakati wa kusaidia upatikanaji wa nishati ya umeme barani Afrika. Mkakati huo ulianzishwa na Rais wa zamani wa Marekani, Barack Obama ukilenga kuhakikisha watu milioni 50 wanafikiwa na umeme katika ukanda wa Jangwa la Sahara barani Afrika ifikapo mwaka 2020.

 

Rusia yatishia kuendelea na mpango wake wa makombora
Mahakama yamfungulia Mdee mipaka