Mahakama Kuu nchini Afrika Kusini imeamuru Rais wa zamani wa nchi hiyo, Jacob Zuma kulipia gharama zote za kesi zilizofunguliwa dhidi yake alipokuwa madarakani.
Mahakama hiyo ya Kaskazini mwa Guateng imeeleza kuwa Zuma atapaswa kulipia gharama zote za uendeshaji kesi zake tangu mwaka 2005 bila kuihusisha Serikali.
“Serikali haihusiki na gharama zozote za kesi dhidi ya Bw. Jacob Zuma, katika mashtaka ya jinai yaliyofunguliwa dhidi yake kwa namna yoyote,” imeeleza sehemu ya uamuzi wa Mahakama Kuu.
“Mwendesha Mashtaka wa Serikali anaelekezwa kufanya majumuisho ya gharama zote zilizoingiwa katika kesi dhidi ya Bw. Zuma ambazo zilikuwa na mashtaka binafsi, ili aweze kukabidhiwa gharama zake kwa ajili ya malipo,” imeongeza.
Chama kikuu cha upinzani cha Democratic Alliance (DA), mwezi Machi mwaka huu kilianza mchakato wa kisheria wa kutaka Zuma alipe kiasi cha $1.3 bilioni ambazo ni pesa za walipa kodi zilizotumika katika kugharamia kesi binafsi dhidi yake alipokuwa madarakani.
Kiongozi wa chama hicho, Mmusi Maimane alisema kuwa kama kuna makubaliano yoyote kati ya Rais Cyril Ramaphosa kuhusu Serikali kulipia gharama hizo ni lazima yawekwe hadharani.