Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), limejiandaa kumjadili Diamond Platinumz baada ya kuelezwa kuwa amekiuka masharti na kuimba wimbo wa Mwanza/Nyegezi katika jukwaa la Wasafi Festival.
Jana, Diamond aliuimba wimbo huo uliofungiwa na Basata, alipokuwa jijini Mwanza ambapo alisindikizwa na Ray Vanny ambaye ni sehemu ya wahusika mkuu kwenye wimbo huo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Basata, Godfrey Mngereza amesema kuwa tayari ameshawasiliana na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Baraza hilo na watatoa tamko lao hivi punde, akieleza kuwa kitendo hicho cha Diamond ni dharau.
“Basata itakuja na majibu muafaka kwa sababu hapa Diamond ameonesha dharau kwa baraza, Bodi, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Serikali kwa ujumla,” Mwananchi inamkariri Mngereza.
Mwanza/Nyegezi ulifungiwa pamoja na video yake Novemba mwaka huu kutokana na kile kilichoelezwa kuwa na maneno ambayo ni kinyume cha maadili ya Kitanzania.