Mbunge wa Arusha mjini, Godbless Lema (Chadema) amesema kuwa endapo Spika wa Bunge Job Ndugai atalithibitishia Bunge kuhusu kauli yake dhidi ya matibabu ya Lissu, yeye atakuwa tayari kujiuzulu.
Ameyasema hayo kupitia ukurasa wake wa Twitter ambapo amejibu kauli iliyotolewa na Spika akiwa bungeni leo ambapo amesema kuwa mpaka sasa bunge limegharamia shilingi milioni 250 katika matibabu ya mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu.
“Bunge halijawahi kumlipia Lissu pesa kwa ajili ya matibabu, alichokisema Mh Spika Ndugai ni upotoshaji kwa jamii. Chama kitatoa tamko juu ya hili. Spika akiweza kuthibitisha hili, mimi nitajiuzulu Ubunge, mshahara wa Mbunge sio hisani ya Spika,”ameandika Lema.
Akizungumza bungeni leo, Januari 31, 2019 Spika Job Ndugai amesema kuwa hadi sasa Bunge limeshamlipa Tundu Lissu shilingi milioni 250 kwa ajili ya matibabu yake.