Luteni Jenerali, Eric Chimese aliyekuwa Mkuu wa Jeshi la Anga la Zambia amefikishwa mahakamani kwa tuhuma za kujihusisha na makosa kadhaa ya jinai ikiwa ni pamoja na ufisadi.
Tume ya Kupambana na Rushwa na Dawa (DEC) imeeleza kuwa Chimese ameshtakiwa pamoja na Mkurugenzi wa Kampuni ya Chita Lodes Limited, James Chungu.
Kwa mujibu wa msemaji wa DEC, Theresa Katongo wawili hao wanatuhumiwa kushirikiana kutoa taarifa za uongo, matumizi mabaya ya ofisi na kumiliki mali ambazo zinadaiwa kuwa za kihalifu.
Rais Edgar Lungu alimfukuza kazi Luteni Chimese mwaka jana bila kueleza wazi sababu za kuchukua hatua hiyo.
East African limeripoti kuwa Luteni Chimese anatuhumiwa kujimilikisha kinyume cha sheria eneo kubwa la ardhi jijini Lusaka na kuliendeleza akiweka majumba tisa ya kifahari yenye eneo la mazoezi la kisasa (gym); na nyumba kadhaa maalum kwa ajili ya wageni. Imeelezwa kuwa alificha umiliki huo na kudanganya kuwa eneo hilo ni mali ya Kampuni ya Chita Lodges.
Chungu mwenye umri wa miaka 51, yeye anashtakiwa kwa kutoa taarifa za uongo kwa vyombo vya dola, ambapo Januari 31, 2019 anadaiwa kukubaliana na maelezo ya Luteni Chimese kuwa eneo hilo linamilikiwa na Kampuni ya Chita Lodge.