Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amezitaka benki nchini kupunguza viwango vya riba zinazotozwa kupitia mikopo mbalimbali wanayoitoa kwa wananchi.
Ameyasema hayo wilayani Hai mkoani Kilimanjaro alipokuwa akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara.
Waziri Mkuu ambaye yuko mkoani Kilimanjaro kwa ziara ya kikazi amesema kuwa kitendo cha benki kutoza riba kubwa kinawaumiza wajasiriamali nchini.
Aidha, Majaliwa amewataka wananchi hususani, vijana, wanawake na wenye ulemavu kuchangamkia fursa ya mikopo inayotolewa katika halmashauri, ambapo amesema kuwa kila halmashauri inatakiwa itenge asilimia 10 ya mapato yake kwa ajili ya kuwawezesha vijana, wanawake na wenye ulemavu kupata mitaji.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka wakulima wa Kahawa wabadilike na kuondoa miti ya zamani na kupanda mipya ili waongeze tija.
Hata hivyo, ameongeza kuwa wakulima hao wanaweza kuweka utaratibu wa kuondoa miche ya zamani kwa awamu na kupanda mipya, hivyo kupata mavuno mengi.