Ubongo ni sehemu muhimu sana katika mwili wa binadamu, ndiyo sehemu inayo ratibu, na kuongoza miitiko ya mwili na matendo yote pia unawezesha mtu kufikiri, kuhifadhi kumbukumbu, na kumfanya ajihisi kuwa ni binadamu.
Kunatabia ambazo zimezoeleka kufanywa na watu wengi lakini hawatambui kuwa ni hatari kwa Ubongo, Mwanasaikolojia Dkt. Edward Ssempira amesema kuwa tabia hizo zisipo chukuliwa hatua haraka zinaweza kusababisha ubongo kupoteza kumbukumbu, ubongo kuharibika na matatizo mbalimbali yatokanayo na ubongo kuharibika.
Muziki wenye sauti kubwa
Katika karne hii ya 21 Vijana wengi hupenda kusikiliza muziki kwa sauti kubwa hasa kwenye kumbi za starehe bila kujua madhara makubwa ambayo ubongo hupata, kwa mujibu wa Dkt. Ssempira, kuna Mahusiano makubwa sana katika ugonjwa wa ukiziwi na ubongo.
Mtu anapo sikiliza Muziki kwa sauti kubwa anasababisha madhara katika ubongo kwani anaupa kazi kubwa ya kufikili na kuelewa kinachosemwa hivyo unashindwa kutunza kumbukumbu.
“Kusikiliza muziki kwa sauti kubwa kwa zaidi ya dakika 30, huharibu ubongo na kunaweza kumpelekea mtu akawa na matatizo ya akili “uzezeta”, hivyo basi tunza usikivu wako ili utunze Ubongo, hii ni kwa kusikiliza Muziki kwa sauti ya chini na kwa wanaosikiliza moja kwa moja kwa kutumia ” Earphones” wasitumie masaa mengi” amesisitiza Dkt. Ssempira.
Kutopata usingizi wakutosha
Kuna ule msemo wa kuhamasisha unaopendwa na wengi kama wengine wanapolala wewe amka, tabia hii ina matatizo kiafya kwani hupelekea hatari ya kusinzia mchana, msongo wa mawazo na kuathili kumbukumbu.
Dkt. Ssempira amesema kuwa kuna sehemu ya Ubongo ambayo huathirika mtu asipopata usingizi wa kutosha, sehemu hiyo ni “Hippocampus”.
“Kuto lala usiku mmoja tu kunapunguza uwezo wa kutunza kumbukumbu mpya na kadri siku zinavyozidi kwenda unakuwa na hatari kubwa ya kupata msongo wa mawazo, sononeko na ugonjwa wa akili au kichaa
Nakusisitiza kuwa kama mtu anapata shida ya kupata usingizi usiku asitumie kahawa, pombe, kuangalia Televisheni na kutumia kompyuta usiku ili aweze kupata usingizi.
Upungufu wa maji mwilini
Kitu cha muhimu kufahamu katika hili ambalo Dkt. Ssempira amesisitiza ni kwamba endapo utahisi kiu ya maji yani ukahisi unahitaji kupitisha maji katika koo lako basi jua tayari una upungufu wa maji mwilini.
Tabia hii ya kunywa maji hadi mtu ahisi kiu imeshakuwa sugu katika jamii bila kujua kuwa ina athari kubwa katika ubongo, kwani huchangia ubongo kuvurugika na kupata tabu katika kufikiri na kufanya kazi zake zaidi ya yute ubongo utapunguza uwezo wa kuwa makini.
Hivyo basi ushauri uliotolewa na Daktari huyu ni kunywa maji sana hasa wakati wa kufanya mazoezi na kipindi cha joto, kwani ni hatari kusubiri hadi uhisi kiu.
Upweke
Tabia ya upweke kwa baadhi ya watu imeonekana ya kawaida japo husababishwa na sababu tofauti tofauti, lakini kama binadamu inashauriwa kuwa na mawasiliano na kuzungumza na binadamu wengine ili kuwa na ubongo wenye Afya.
Dkt, Ssempira ameeleza kuwa kujitenga na kuwa mpweke kuna ongeza hatari ya akili kufanya kazi kwa udhaifu, msongo wa mawazo na hata kupelekea ubongo kuvurugina na ukichaa.
Imeelezwa kuwa watu walio na marafiki wana uwezekano mdogo wa kupata maradhi ya akili na ubongo wao hufanya kazi kwa ufasaha.
Hizo ni baadhi ya tabia hatarishi kwa ubongo wa Binadamu japokuwa zipo nyingi kama kutopata mwanga wa jua wa kutosha na kuishi kwenye mazingira machafu.