Kocha wa Klabu ya Real Madrid, Santiago Solari ametoa kejeli na vicheko kuhusu tetesi kuwa Kocha wa zamani wa Manchester United, Jose Mourinho anaweza kuchukua kibarua chake hivi karibuni.
Hatua hiyo imekuja ikiwa ni siku mbili tangu Mourinho azungumzie uwezekano wa kukinoa tena kikosi cha Real. Solari ambaye ameonesha kuchekelea tetesi hizo, amedai kuwa klabu hiyo imewahi kuwa na waigizaji zaidi ya wale wa Hollywood, akimtaja mrembo Julia Roberts (pichani).
“Klabu hii imewahi kuwa na waigizaji wengi zaidi ya Julia Roberts,” alisema Salari. Julia ni muigizaji nguli wa kike wa Marekani, maarufu zaidi katika tamthilia za mapenzi.
Uchokozi wa waandishi wa habari kuhusu jina alilolitaja ulienda mbali na kumuuliza ni nani kati yake na Mourinho ambaye Julia angemchagua ili ale naye bata.
“Katika sekta hiyo, ingepaswa kumuuliza yeye [Julia] mwenyewe,” alijibu.
Wikendi iliyopita, Mourinho ambaye hivi sasa hana kibarua baada ya kutimuliwa na Manchester United Desemba mwaka jana, aliiambia beIN SPORTS kuwa yuko tayari kurejea Real Madrid katika siku za usoni.
Real Madrid inatarajia kukikwaa kisiki cha Ajax leo usiku, na Solari amedai kuwa watafanya vizuri na kwamba wachezaji wake wamejipanga kuhakikisha pengo la Cristiano Ronaldo linabaki kuwa historia nzuri.